1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatajwa kuwa na mahusiano ya karibu na Hamas

Mathias Bölinger/Mohammed Khelef17 Agosti 2016

Waraka uliopewa jina 18/9274 una maswali 19 yanayoulizwa na kundi la wabunge wa chama cha die Linke kuhusu majaribio ya serikali ya Uturuki kusaka ushawishi miongoni mwa wanasiasa wa Kijerumani.

https://p.dw.com/p/1JjUy
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: Getty Images/AFP/A. Nemenov

Maswali kama haya huulizwa mara kwa mara bungeni na chama kinachoelemea siasa za mrengo wa shoto, die Linke, kimekuwa kikija na matakwa magumu dhidi ya Uturuki, ila waraka huu una umuhimu wa kipekee.

Siku moja baada ya kuwasilishwa bungeni, wanajeshi walifanya jaribio la mapinduzi nchini Uturuki na katika kipindi hiki cha kuwaandama wanaoshukiwa kuhusika na jaribio hilo, nyufa kati ya serikali kuu Berlin na ile ya Ankara sasa zinaonekana wazi.

Suala lenyewe ghafla likaja juu kwa kila mtu kuliona. Wafuasi wa Rais Tayyip Erdogan waliandamana mjini Cologne, na suala la mpasuko baina ya pande hizi mbili juu ya ruhusa ya kusafiri pasina viza kwa raia wa Uturuki likazuka.

Pakazuka pia mashaka endapo taasisi ya masuala ya kidini ya Uturuki, DITIB, inafanya kazi zake ndani ya misikiti nchini Ujerumani. Masuali yote haya ambayo yana maslahi ya moja kwa moja kwa umma, yaliibuliwa katika kipindi hiki kigumu.

Majibu ya serikali yafadhaisha

Jambo linalofadhaisha zaidi ni majibu kutoka serikali kuu ya shirikisho, kwamba kwa sababu za kiusalama, isingeliwezekana kuyajibu maswali hayo. Takribani kila jawabu kutoka kwa msemaji wa wizara ya mambo ya ndani bungeni, Ole Schroeder, lilikuwa hilo hilo moja kwa kila swali.

Wakati mwengine alikuwa hata anakusanya maswali manane kwa pamoja na kuyapa jawabu moja: “Kwa sababu hizi, Serikali Kuu ya Shirikisho haiwezi kutoa taarifa zinazoweza kusambazwa kupitia vyombo vya habari.” Alikuwa akisema.

Lakini moja ya mambo ya kufurahisha kwenye kiambatanisho kimoja kilichotumwa na kuripotiwa kwenye studio za televisheni ya ARD, na ambacho kiliwekwa alama ya “kwa matumizi ya ofisi tu”, kikikusudiwa kuwa kisitangazwe hadharani, ni sehemu ya siri ya majibu ya swali mojawapo. Sehemu hiyo inasema: “kuna mkaribiano wa kiitikadi kati ya hotuba za chama cha AKP cha Erdogan na kile cha Udugu wa Kiislamu.”

Msemaji wa wizara ya Mambo ya ndani ya Ujerumani kwenye bunge la Ujerumani, Ole Schroeder.
Msemaji wa wizara ya Mambo ya ndani ya Ujerumani kwenye bunge la Ujerumani, Ole Schroeder.Picha: picture alliance/dpa

Waraka huo unasema pia kuwa mafungamano kati ya Uturuki na Hamas na chama cha Udugu wa Kiislamu cha Misri yameimarika maradufu chini ya uongozi wa Erdogan. Kwamba Uturuki imekuwa jukwaa kuu la upangaji mikakati kwa makundi ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati, kiasi cha kwamba televisheni nyingi za satalaiti za Udugu wa Kiislamu zinarusha matangazo yake ndani ya ardhi ya Uturuki.

Na hili ni lile linaloitwa bomu kwenye siasa za Ujerumani, kwa sababu kumbe kwa miaka mingi idara za ujasusi za Ujerumani zilijuwa kuwa kuna ukaribu mkubwa kati ya serikali ya Uturuki na chama cha Hamas, ambacho Ujerumani inakichukulia kuwa ni kundi la kigaidi.

Hili linakipa nguvu chama cha die Linke kwenye hoja yake ya muda mrefu, kwamba serikali ya Kansela Angela Merkel imekuwa na sera laini sana kuelekea Uturuki, na kama anavyosema mmoja wa makada wakubwa wa chama hicho, Sevim Dagdelen, mwenyewe akiwa na asili ya Uturuki: “Ni jambo la kutisha kuwa hata baada ya yote hayo, serikali ya Erdogan hupigwa kwa mito ya usufi tu.”

Mwandishi: Mathias Bölinger
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba