Uturuki yashupalia madai yake juu ya kundi la YPG
18 Februari 2016Hadi wakati huu wizara ya mambo ya nje haijaweza kuthibitisha tukio hilo ambalo limeripotiwa na shirika la habari la NTV la Uturuki.
Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu awali alisema ushahidi kuhusu mashambulio ya jana mjini Ankara utajadiliwa pamoja na nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Ama kwa upande mwingine kuhusiana na mashambulio yanayofanywa na Uturuki dhidi ya waasi wa kikurdi kundi kubwa la wanamgambo wakikurdi nchini Syria limeshasema kwamba halihuki kabisa na mashambulio yaliyofanywa katika mji mkuu wa Uturuki Ankara likiongeza kwamba madai yanayotolewa na waziri mkuu Davutoglu ni uwongo unaodhamiriwa kufungua njia ya kuhalalisha mashambulizi ya Uturuki dhidi ya maeneo ya wakurdi nchini Syria.
Kundi hilo la wanamgambo wakikurdi wa Syria linalofahamika kama YPG limeeleza kwamba dhima yake kubwa imekuwa ni kuwalinda watu wake dhidi ya magenge yanayofanya unyama nchini Syria likikusudia wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislamu pamoja na makundi yanayofungamana na al Qaeda.Mapema hii leo waziri mkuu Davutoglu alisema kwamba nchi yake italipiza kisasi dhidi ya kundi la YPG ambalo amelitwika dhamana ya mashambulizi ya bomu mjini Ankara yaliyosababisha watu 28 kuuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Taaarifa ya YPG lakini imesisitiza kwamba kundi hilo halijiingizi katika shughuli zozote za kijeshi dhidi ya nchi yoyote jirani au kundi lolote.Limekwenda mbali zaidi kundi hilo na kusema kwamba pamoja na vitendo vya uchokozi na mashambulio yanayofanywa na Uturuki dhidi ya maeneo ya wakurdi nchini Syria halijawahi hata mara moja kuthubutu kulipiza kisasi dhidi ya Uturuki.
Wakati huohuo serikali ya Ujerumani imefahamisha kwamba Kansela Angela Merkel amezungumza na viongozi wa Uturuki na kutoa rambirambi zake baada ya tukio la mashambulizi ya Ankara yaliyowalenga wanajeshi.Kansela Merkel amelaani kwa nguvu zote mashambulio hayo na kuwahakikishia viongozi wa Uturuki kwamba nchi yake itakuwa pamoja na Uturuki katika mshikamano wa vita dhidi ya ugaidi.
Rais Recep Tayyip Erdogan anashikilia kwamba licha ya waasi wa kikurdi kukanusha kuhusika na mashambulizi ya Ankara kuna ushahidi unaothibitisha kwamba waasi hao walioko Syria wanabeba dhamana ya mashambulizi hayo ya bomu la kutegwa ndani ya gari mjini Ankara.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Daniel Gakuba