Uturuki yashambulia maeneo ya magaidi Iraq na Syria
13 Januari 2024Uturuki imefanya karibu mashambulizi 30 ya anga usiku kucha kwenye "miundombinu ya magaidi" kaskazini mwa Iraq na Syria katika mikoa ya Metina, Hakurk, Gara na Qandil.
Soma pia: Uturuki yawaandama PKK kufuatia mashambulizi Ankara
Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imesema mashambulizi hayo yamefanyika baada ya vifo vya wanajeshi tisa wa nchi hiyo waliouwawa katika kambi moja ya jeshi huko Iraq.
Taarifa ya wizara hiyo imefafanua kuwa mashambulizi ya anga ya Ankara yalilenga maeneo 29 yakiwemo mapango, malazi, mahandaki na mitambo ya mafuta ambayo ni mali ya chama cha wafanyakazi cha Wakurdi PKK pamoja na kundi la wanamgambo la YPG la Syria.
Ankara imekuwa ikiendesha vituo kadhaa vya kijeshi kwenye eneo hilo kwa miaka 25 iliyopita katika vita vyake vya miongo mingi dhidi ya PKK, kundi lililoorodheshwa na Uturuki na washirika wake wengi wa mataifa ya magharibi kuwa ni la kigaidi.