Uturuki yasema iko tayari kwa mazungumzo na Ugiriki
26 Agosti 2020Waziri wa Mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema nchi yake inakubali pendekezo la kuwepo mazunguzo yasiyo na masharti juu ya uwezekano wa kugawana kwa usawa rasilimali zilizopo kwenye eneo hilo la bahari.
Mvutano huo umeshuhudia mataifa hayo mawili jirani yakitunishiana misuli kwa kufanya luteka za kijeshi.
Msimamo wa Uturuki umetolewa baada ya juhudi za waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas ambaye jana alizitembelea Uturuki na Ugiriki kujaribu kutuliza mzozo unaofukuta.
Ugiriki nayo imesema itakubali kushiriki majadiliano ya kutafuta suluhu ya mzozo unaondelea lakini siyo chini ya vitisho kutoka Uturuki.
Hayo yamesemwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ugiriki Nikos Dendias baada ya kufanya mkutano na Maas mjini Athens.
Maas amepata ahadi chache za kutia moyo kutoka pande hizo mbili, ambazo bado zinarushiana maneno kuhusu suala la mzozo unaoendelea.
Maas: Hali ya mzozo inatia wasiwasi
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake nchini Ugiriki na Uturuki, Maas ameonya kuwa mzozo kati ya mataifa hayo mawili wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO umefikia kiwango cha kutia mashaka.
"Tunachohitaji sasa na kwa haraka ni hatua za wazi kuelekea kupunguza mvutano na pia nia ya dhati ya kuingia kwenye majadiliano. Nimesikia hilo kuwa kila upande uko tayari kwa mazungumzo. Na ndiyo maana tunaamini kuwa nia hiyo inaweza kufikiwa. " amesema Maas.
Uturuki imesifu juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Ujerumani lakini amesema yenyewe ilikwishaonesha nia njema, ilipositisha shughuli za utafutaji gesi na mafuta kwenye eneo linalozozaniwa mnamo mwezi uliopita.
Kulingana na waziri wake wa mambo ya kigeni, Uturuki ililazimika kuanza tena shughuli hizo baada ya Ugiriki kusaini mkataba na Misri wa kuunda kanda maalum ya uchumi katika eneo la bahari lenye mzozo.
Umoja wa Ulaya kujadili mvutano unaoendelea
Ahadi za uwezekano wa kufanyika mazungumzo zimetolewa kuelekea mkutano usio rasmi wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika mjini Berlin, siku Alhamisi na Ijumaa.
Ugiriki inatarajiwa kuwashinikiza viongozi wa kanda hiyo kuiwekea vikwazo Uturuki lakini mataifa ya Umoja wa Ulaya bado yanajizuia kuchukua hatua hiyo yakihofia kuikasirisha Uturuki, ambayo mshirika muhimu wa Jumuiya ya NATO.
Uturuki na Ugiriki zinawania udhibiti wa eneo la mpaka wa bahari ya Mediterannia unaoaminika kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta na gesi asili.
Ugiriki inasema utafutaji wa rasilimali hizo unaofanywa na Uturuki ni kinyume cha sheria, huku Uturuki ikidai eneo inalotumia ni sehemu ya mipaka yake ya baharini.