Chama cha Kikurdi chasema waliouawa ni 128
12 Oktoba 2015Hatua hiyo inakuja mnamo wakati serikali nchini humo ikisema idadi ya watu waliouwawa katika tukio hilo hadi sasa ni 97 na kusema miongoni mwao ni raia wa palestina. .
Chama cha wafuasi wa kikurdi tayari kimesema ya kuwa kiasi cha watu 128 waliuawa katika shambulizi hilo la jumamosi lililotokea nje kidogo ya kituo kikuu cha treni mjini Ankara ambalo linadaiwa kuwa lilikuwa linawalenga wanaharakati wa kituruki na kikurdi ambao walikuwa wamekusanyika katika mkutano uliokuwa na lengo la kuhimiza demokrasia na kukomesha mapigano kati ya waasi wa kikurdi na vikosi vya usalama nchini humo.
Mapigano hayo hadi sasa yamesababisha vifo vya mamia ya watu nchini humo katika kipindi cha tangu mwezi July mwaka huu.
Baadhi wamshutumu Rais Erdogan kwa kuchochea vurugu.
Serikali nchini humo imesema ya kuwa waasi wa kikurdi au wanamgambo wa kundi la dola la kiisilamu wanaweza kuwa wanahusika, wakati wa ombolezaji wa tukio hilo wakimshutumu rais Recep Tayyip Erdogan kwa kuchochea vurugu ili kuweza kujipatia kura nyingi kupitia chama tawala kuelekea katika uchaguzi ujao wa Nov 1.
Mmoja wa watu nchini humo alisikika akisema kuwa watu sasa wanaanza kukata tamaa katika harakati za ,kutafuta amani nchini humo.
Hakuna mtu au kundi lolote ambalo hadi sasa limethibitisha kuhusika na mlipuko huo lakini serikali imekuwa ikilishutumu kundi la dola la kiisilamu amablo liliwaua wanaharakati wa masula ya amani wa kituruki na kikurdi wapatao 33 mwezi Julai mwaka huu katika mji wa Suruc ulioko mpakani mwa Syria.
Gazeti moja nchini humo liitwalo Hurriyet nchini humo limeripoti kuwa aina ya vifaa vilivyotumika katika tukio la milipuko hiyo ni sawa na vile vilivyotumika katika tukio la Suruk.
Gazeti la Yeni Safak, ambalo ni gazeti linalofahamika kuwa karibu zaidi na serikali ya nchi hiyo limeripoti ya kwamba wachunguzi wa tukio hilo walikuwa wanafanya majaribio ya sampuli za vina saba vilivyopatikana katika familia za waturuki 20 ,wanaoaminika kuwa wanamgambo wa kundi hilo la dola la kiisilamu wanaodaiwa kuhusika na milipuko hiyo.
Hapo jana polisi nchini humo waliwatia mbaroni watuhumiwa wengine wanne zaidi wa kundi hilo la dola la kiisilamu katika msako uliofanywa katika mji wa kusini wa Adana. Hatua hiyo inafanya idadi ya watu ambao ni washukiwa wa kundi la dola la kiisilamu waliokwisha tiwa mbaroni hadi sasa kufikia 40.
Mwandishi: Isaac Gamba/APE
Mhariri :Yusuf Saumu