Uturuki yafanya mazungumzo na pande zote Afghanistan
17 Agosti 2021Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ameyasema hayo baada ya vyanzo vya kiusalama vya Uturuki kudai kuwa Ankara imefuta mipango yake ya kuulinda uwanja wa ndege wa Kabul kufuatia kuondolewa kwa majeshi zaidi ya vikosi vya Jumuiya ya kujihami ya NATO kutoka Afghanistan kwasababu ya ushindi wa Taliban.
Vyanzo hivyo vimelieleza shirika la habari la Reuters kwamba Uturuki nchi ya Kiislamu ambayo ina moja ya vikosi vikubwa vya NATO, ilikuwa tayari kutoa msaada wa kiufundi na kiusalama ikiwa kundi la Taliban litaomba usaidizi. Awali kundi hilo liliionya Uturuki juu ya kubakisha vikosi vyake mjini Kabul kwa ajili ya kulinda uwanja wa ndege lakini maafisa walisema kuwa hawakuvitaka vikosi vya Uturuki kuondoka Afghanistan, wakiwa na matumaini ya kuimarisha ushirikiano na mataifa ya Kiislamu na kutambulika kimataifa. Zaidi waziri Cavusoglu anasema kuwa
"Hivi sasa Waafghan watajadili masuala yote miongoni mwao. Nani atakuwamo katika serikali ya mpito! Ni aina gani ya serikali ya mpito wanaitaka. Tutaona na kujadili yote haya. Lakini kwanza nchi inahitaji kuwa na utulivu."
Kwa upande wake Urusi nayo imesema kuwa tangu Taliban wakamilishe udhibiti kamaili wa kijeshi, wameonyesha mwenendo wenye "ishara chanya" na kwamba inaunga mkono mdahalo "jumuishi" wa kisiasa katika nchi hiyo. Waziri wake wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov amesema Taliban, wanaashiria "utayari wa kuheshimu maoni ya wengine".
"Tunaunga mkono kuanza kwa mchakato wa mdahalo wa kitaifa ambao ni jumuishi ambao utashirikisha pande zote za kisiasa za Afghanistan, makabila na makundi yote ya kidini". Awali Moscow ilisema kuwa itaitambua serikali mpya ya Taliban kwa kuzingatia ni jinsi gani utawala mpya utakavyoongoza.
Uzberkistan ambayo ni jirani na Afghanistan nayo imedai kufanya mazungumzo na Taliban na imeonya kwamba "itazima vikali" jaribio lolote la kukiuka haki zake za mipaka baada ya ghasia za mjini Kabul kusambaa hadi katikati mwa Asia. Uzberkistan imetoa taarifa hiyo baada ya kushuhudia vikosi vya Afghanistan vikivuka mpaka kiharamu na kuingia nchini humo wakati vikijaribu kuwakimbia wapiganaji wa Taliban.
Wakati huohuo Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Mueller amelieleza gazeti la kila siku la Ujerumani- Rheinische Post kwamba "misaada ya kimaendeleo inayoendeshwa na serikali kwa sasa imesimamishwa." Shirika la habari la Ujerumani dpa limeripoti kwamba hadi kufikia sasa Afghanistan ilikuwa ndio nchi iliyopokea misaada mingi ya maendeleo kutoka Ujerumani duniani kote.