Uturuki: Maandalizi ya mashambulizi Syria yamekamilika
8 Oktoba 2019Uturuki imesema, imekamilisha maandalizi ya mashambulizi Kaskazini mwa Syria, baada ya ishara zenye mkanganyiko za Marekani kuhusu iwapo itaruhusu operesheni ya kijeshi. Haya ni baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuamuru vikosi vyake kuondoka katika eneo la mpaka wa Syria.
Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan, ametishia mara kadhaa kuwashambulia wanamgambo wa Kikurdi katika eneo la mpaka Kaskazini mwa Syria. Hii ni kutokana na uhusiano wa wanamgambo hao na watu wanaotaka kujitenga chini mwake. Wizara ya Ulinzi ya Uturuki, ilitoa taarifa ya kukamilika kwa maandalizi ya mashambulizi Kaskazini mwa Syria kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Awali, Rais Erdogan alisema mashambulizi hayo ya kijeshi yanaweza kufanyika wakati wowote bila kutoa ilani. Hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump, ya kuviondoa vikosi vyake Kaskazini mwa Syria imekosolewa vikali na wakosoaji wanaoiona kama kuviacha vikosi vya Wakurdi ambavyo vimekuwa mshirika muhimu katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita dola la Kiislamu IS.
Tangazo la Trump la kuviondoa vikosi vyake limepata pia upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa chama cha Democratic pamoja na chama chake cha Republican wakionya kuwa shambulio lolote la Uturuki litasababisha mauaji ya halaiki ya Wakurdi ambao wanawashikilia wapiganaji wa kundi la IS pamoja na familia zao.
Uturuki haitojibu mapigo kutokana na vitisho
Kwa upande wake makamu wa Rais wa Uturuki Fuat Oktay amemjibu Trump hii leo akionya kuwa Taifa lake halitojibu mapigo kutokana na vitisho.
Amesema, kama ambavyo Rais Erdogan husisitiza, Uturuki itashika njia yake na kushughulikia mambo yake yenyewe. Uturuki inasema, inataka eneo salama Kaskazini mwa Syria ili lisiwe maficho ya vikosi vya Kikurdi na kuruhusu karibu wakimbizi milioni mbili wa Syria kurejea nyumbani.
Wakati huohuo, Mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Uturuki, yamewalenga wanamgambo wa kikurdi Kaskazini mwa Iraq katika maeneo ya Hakurk na Hafta. Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya Uturuki na kwamba "magaidi" tisa wameuawa katika tukio hilo.