1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kuwa mpatanishi kati ya Ethiopia na Sudan

Sylvia Mwehozi
19 Agosti 2021

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameunga mkono azimio la amani kuhusu mzozo wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia na kuwa mpatanishi baina ya Ethiopia na Sudan katika mzozo tofauti wa mpaka.

https://p.dw.com/p/3z9xw
Türkei Präsident Recep Tayyip Erdogan
Picha: Aytac Unal/AA/picture alliance

Rais Erdogan ameyazungumza hayo wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye alikuwa ziarani Uturuki.

Ziara ya Abiy inakuja katikati mwa mzozo unaozidi kutokota huko Tigray ambao ulianza mwezi Novemba baada ya mzozo wa kisiasa baina ya waziri huyo mkuu na viongozi wa mkoa wa Tigray, ambao walikuwa wametawala serikali ya Ethiopia kwa karibu miongo mitatu.

Maelfu ya watu wameuawa katika vita ya Tigray iliyodumu kwa miezi tisa sasa  na kuwepo na kuenea kwa madai ya ubakaji kutoka magenge ya Watigray  na kufukuzwa watu wa Tigray kunakofanywa na vikosi vya Ethiopia na washirika wake. Erdogan ameongeza kuwa amani, utulivu na uadilifu wa Ethiopia, ambao ni eneo la kimkakati una umuhimu mkubwa barani Afrika, na kwa Uturuki.

"Ethiopia inapitia kipindi nyeti. Tulijadili maendeleo na hali ya hivi karibuni katika mkoa wa Tigray.Tunaona umuhimu mkubwa katika utatuzi wa shida zilizopo katika mfumo wa utulivu na uhifadhi wa amani na utulivu katika eneo hili" alisema Erdogan.

Türkei | Recep Tayyip Erdogan - Abdel Fattah al-Burhan | Treffen in Ankara
Abdel Fattah al-Burhan (kulia) na rais wa Tayyip ErdoganPicha: Emin Sansar/AA/picture alliance

Aidha Rais Erdogan pia aligusia utayari wa Uturuki kuwa mpatanishi kati ya Ethiopia na Sudan ili kuutatua mzozo mwingine tofauti unaohusiana na mpaka kati ya nchi mbili hizo.

Rais Erdogan ambaye wiki iliyopita alikuwa mwenyeji wa mwenyekiti wa baraza la Sudan Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan ameongeza kuwa Uturuki imejiandaa kutoa mchango wake katika upatikanaji wa suluhisho la amani juu ya mzozo baina ya Ethiopia na Sudan juu ya mkoa wa Al-Fashaga.

Hapo jana rais wa Uturuki na Waziri Mkuu wa Ethiopia walitia saini makubaliano ya kijeshi pamoja na ushirikiano wa kifedha kwa majeshi ya pande hizo mbili.

Nalo shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake iliyotolewa Jumatano kuwa watoto wadogo ni miongoni mwa wanaoathirika katika wimbi jipya la kukamatwa na kuzuiwa kwa raia wa Tigray wanaoshukiwa kuviunga mkono vikosi vya mkoa huo katika vita vinavyozidi kuongezeka nchini Ethiopia.

Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, mmoja wa watu wanaoshikiliwa ameyaelezea mazingira hafifu ambako zaidi ya watu 700 wa jeshi la Tigray, familia zao na wastaafu wanashikiliwa katika kambi moja kwenye mkoa wa Oromia.