Uturuki kutuma vikosi vya jeshi Libya
27 Desemba 2019Waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte na rais wa Urusi Vladimir Putin hata hivyo wametoa wito wa kupatikana suluhisho la mzozo huo kwa njia ya amani.
Serikali ya Libya inayotambulika kimataifa serikali ya maridhiano ya kitaifa GNA mjini Tripoli imekuwa ikihangaika kuzuwia majeshi ya mbabe wa kivita jenerali Khalifa Haftar, ambayo yamekuwa yakiungwa mkono na Urusi, Misri, Umoja wa falme za Kiarbu UAE na Jordan.
Afisa mjini Tripoli amethibitisha kutolewa ombi rasmi kwa msaada wa majeshi ya Uturuki angani, ardhini na baharini.
Afisa huyo , ambaye hakutaka kutajwa jina , amezungumza baada ya waziri wa mambo ya ndani wa serikali ya mjini Tripoli, Fathi Bashagha , kuashiria katika maelezo kwa waandishi habari mjini Tunis kuwa hakuna ombi kama hilo lililotolewa.
" Serikali ya maridhiano ya kitaifa imetia saini taarifa ya makubaliano na serikali ya Uturuki chini ya msingi wa ombi kutoka Uturuki. Tunaamini kuwa kutakuwa na ushirikiano mkubwa na Uturuki, Tunisia, na Algeria, na tutakuwa katika ushirika katika njia kwamba unawanufaisha watu wetu na uthabiti wa usalama wetu, pamoja na uchumi ambao ni chanzo cha wasi wasi kwetu sote. ushirikiano wa kiuchumi unahitaji uthabiti katika usalama pamoja na uthabiti wa kisiasa."
Marekani afanya mazungumzo na Sisi
Majeshi ya Haftar yameshindwa kufika katikati ya Tripoli lakini yamepata mafanikio madogo katika wiki za hivi karibuni katika baadhi ya maeneo ya nje ya mji huo upande wa kusini kwa msaada wa wapiganaji kutoka Urusi na Sudan, pamoja na ndege zisizo na rubani zilizoingizwa na Umoja wa Falme za kiarabu, UAE, wanadiploamsia wamesema.
Rais wa Marekani Donald Trump jana alifanya mazungumzo ya simu na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, ikulu ya Marekani ya White House imesema, ambapo viongozi hao wawili walikataa kile walichosema kuwa ni mataifa ya nje kuitumia Libya.
Uturuki tayari imekwisha tuma vifaa vya kijeshi kwa serikali hiyo maridhiano ya kitaifa licha ya vikwazo vya silaha vya Umoja wa mataifa kwa Libya , kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa mataifa iliyopatikana na shirika la habari la Reuters mwezi uliopita.
Rais wa Urusi Vladimir Putin na waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte walikubaliana jana kuwa hali nchini Libya inapaswa kutatuliwa kwa njia ya amani, ikulu ya urusi Kremlin imesema.