1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kuandaa mkutano wa kuijadili Syria

Amina Abubakar Gakuba, Daniel
22 Agosti 2019

Msemaji wa rais wa Uturuki Ibrahim Kalin amesema rais Erdogan atakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa viongozi wezake kutoka Iran na Urusi wa kuujadili mgogoro wa Syria mjini Ankara mnamo Septemba 16

https://p.dw.com/p/3OL2y
Türkei Bursa | Recep Tayyip Erdogan, Präsident - Eröffnung einer Autobahn
Picha: Reuters/Cem Oksuz/Presidential Press Office

Tangazo la kufanyika mkutano kati ya rais Vladimir Putin wa Urusi, rais wa Iran Hassan Rouhani na Erdogan linakuja wakati ambapo vikosi vya Syria vimepiga hatua katika ngome ya mwisho ya waasi mjini Idlib Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Urusi na Iran wanaoiunga mkono serikali ya Syria wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na Uturuki kujaribu kupata suluhu la mgogoro huo uliodumu zaidi ya miaka mitano, licha ya kuwa inaunga mkono upinzani katika mgogoro huo.

"Rais atakuwa na mkutano wa kilele utakaohudhuriwa na mataifa matatu, mwenyeji Uturuki Urusi na Iran," alisema msemaji huyo wa rais Erdogan, Ibrahim Kalin.

 Vita vya mara kwa mara vinavyoendelea huko vinaipa wasiwasi Uturuki kuwa wimbi kubwa la wakimbizi katika eneo hilo lililo na idadi ya watu milioni tatu huenda wakakimbilia nchini Uturuki.

Türkei Ankara Ibrahim Kalin Sprecher des Präsidenten
Msemaji wa rais wa Uturuki, Ibrahim Kalin.Picha: picture-alliance/AA/M. Ali Ozcan

Marais hao watatu watauzungumzia mji wa Idlib katika mkutano wao ujao pamoja na kuundwa kwa tume ya kushughulikia katiba mpya na namna mchakato wa kisiasa unavyopaswa kuendelea.

Mkutano wa mwisho wa kutafuta suluhu katika Mgogoro wa Syria ulifanyika mwezi Februari na mkutano wa mwezi Septemba mwaka huu utakuwa mkutano wa tano wa kilele kati ya rais Vladimir Putin wa Urusi, Hassan Rouhani wa Iran na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki tangu mwezi Novemba mwaka 2017.

Msemaji wa Rais Erdogan amesema katika siku za hivi karibuni rais huyo atazungumza na rais Putin kupitia njia ya simu akiongeza kuwa matayarisho yanaendelea ya kuwa na mazungumzo mengine kwa njia ya simu na rais wa Marekani Donald Trump.

Chanzo: afp