1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan kukutana na trump

12 Mei 2017

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amepinga uamuzi wa Marekani kuwapa silaha wanamgambo wa Kikurdi nchini Syria katika harakati zao za vita dhidi ya kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.

https://p.dw.com/p/2ct8r
Türkei Präsident Erdogan
Picha: Reuters/A. Zemlianichenko/Pool

Hata hivyo, akizungumza katika uwanja wa ndege wa Ankara alipokuwa njiani akielekea China kwa mazungumzo ya kiuchumi na baadaye Marekani kukutana na Rais Doanld Trump, Erdogan alisema Uturuki inajaribu kuifahamu zaidi Marekani kwa vile bado nchi hiyo iko katika mchakato wake wa mabadiliko katika uongozi wake.

Ikulu ya Marekani ilitangaza wiki hii kwamba itawapa silaha kundi la wanamgambo wa Kikurdi wa YPG nchini Syria, ambacho kinakaribia sehemu ya al- Raqqa ambao ndio mji mkuu wa kikundi cha Dola la Kiislamu.

Marekani imekuwa ikuwaunga mkono kundi hilo la wanamgambo wa kikurdi tangu 2014 na pia wana majeshi yao katika sehemu ya ya mashariki ya eneo linalozuiliwa na kundi hilo. Pia urusi

inaunga mkono kundi hilo katika sehemu ya Kaskazini maghribi ya Syria.

Hata hivyo, serikali mjini Ankara inaliona kundi la YPG  kuwa ni kundi la kigaidi lisilopaswa kusaidiwa kwa silaha, ingawa maafisa wa Marekani wamesisitiza kuwa watatumia silaha zao katika kupambana na makundi yenye itikadi kali za Kiislamu.

Syrien YPG in Rakka
Kikundi cha wanamgambo wa YPG wakiwa RakkaPicha: picture-alliance/dpa/S. Suna

Kabla ya ziara ya Erdogan, kiongozi wa kundi la Wakurdi nchini Syria, Sinam Mohamed, amechapisha makala katika gazeti la The New York Times na kuitaka Marekani isiache kuliunga mkono kundi hilo, hata kama itashinda vita dhidi ya IS akiongeza kuwa "YPG haina mpango wa kupambana na Uturuki, bali kuanzisha demokrasia changa kaskazini mwa Syria kwa msingi wa shirikisho."

Matumaini ya muafaka na Trump

USA Präsident Donald Trump im Weißen Haus
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Kiongozi huyo wa Uturuki amesema kuwa ana matarajio kuwa mkutano wake na Trump utakuwa

muhimu katika maamuzi mbali mbali.

Sauti ya kiongozi huyo wa Uturuki juu ya Marekani, ambaye amekuwa na jitahada kubwa kutaka Marekani kutowaunga mkono Wakurdi nchini Syria, inafanana sasa na ile aliyotumia juu ya Ulaya hivi karibuni.

Wakati wa kampeni zake za kwenye kura ya maoni ya kumuidhinishia madaraka makubwa zaidi, Erdogan alisema viongozi wengi wa Ulaya walikuwa na tabia kama ya Wanazi na mafashisti. Kiongozi huyo wa Uturuki pia alionekana hivi karibuni kutumia istilahi ya Trump juu ya Jumuiya ya Kujihami yaani NATO.

Brüssel Nato-Hauptquartier
Makao makuu ya Jumuiya ya Kujihami NATO mjini BrusselsPicha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

 

 

"Ikiwa NATO haitafanya wajibu wake wa kupigana na ugaidi, kuna haja gani ya kuwepo kwa jumiya hii? Tutazungumzia juu ya hili pia." Erdogan alisema katika mkutano na waandishi wa habari.

Rais Trump alipokuwa akifanya kampeni ya kugombea urais alisema pia kulikuwa hakuna umuhimu wa kuwepo kwa NATO, ingawa aliibadilisha kauli hiyo mwezi uliopita, akisema kuwa jumuiya hiyo imebadilika na sasa wanapigana dhidi ya ugaidi.
 

NATO itakuwa na mkutano wa kilele mjini Brussels mwisho wa mwezi huu, ambapo Trump na Erdogan wanatarajiwa kuhudhuria.

Erdogan kumtaka Trump amrejeshee Gullen

Katika mkutano ujao baina ya rais Erdogan na Trump, Erdogan anatarajia kuzungumzia juu ya

ulamaa wa Kituruki anayeishi uhamishoni nchini Marekani, Fethullah Gulen, ambaye anadaiwa  kushiriki katika jaribio lililoshindwa la kuipindua serikali ya Uturuki mwaka jana.

Erdogan atazamiwa kumkabidhi Trump ombi rasmi la kutaka Gullen arejeshwe Uturuki, lakini serikali ya mtangulizi wa Trump, Barack Obama, iliwahi kulikataa ombi hilo, ikisema kwamba hakukuwa na uthibitisho wa tuhuma hiyo.

"Tutalishughulikia hili hadi tulitie mwisho," alisema Erdogan.

Mwandishi: Najma Said/DPAE/ECA

Mhariri: Mohammed Khelef