Utulivu warudi New Delhi baada ya ghasia kuuwa watu 20
26 Februari 2020Askari wa kutuliza fujo wameonekana mitaani katika mji huo mkuu wa India hivi leo, baada ya siku mbili za machafuko ambayo yameshuhudia makundi ya watu waliojihami kwa panga na bunduki wakikabiliana, katika kile kinachotajwa kuwa ghasia mbaya kabisa za kidini kuwahi kushuhudiwa mjini Delhi kwa miongo kadhaa sasa.
Akivunja ukimya wake juu ya ghasia hizo, Waziri Mkuu Narendra Modi, ambaye wakosoaji wanamchukulia kuwa ndiye chanzo kikuu cha machafuko haya kupitia sheria iliyopendekezwa na serikali yake, ametoa wito wa amani kwenye mji huo wenye wakaazi zaidi ya milioni 18. "Amani na masikizano ndiyo msingi wa maadili yetu. Nawaomba kaka na dada zangu wa Delhi kutunza amani na udugu muda wote," alisema siku ya Jumatano (Februari 26).
Waziri Kiongozi wa Delhi, Arvind Kejriwal, amesema jeshi linapaswa kupelekwa kwenye mji huo na marufuku ya kutotoka nje iwekwe kwenye wilaya zenye machafuko makubwa upande wa kaskazini mashariki mwa mji huo mku. Kupitia ujumbe wake wa Twitter, Kerjiwal ameandika hivi leo kwamba polisi pekee haiwezi kudhibiti hali.
Polisi walishindwa kuzuwia machafuko
Kauli ya waziri kiongozi huyo inasadifiana na za manusura wa mapigano hayo ambao wameliambia shirika la habari la AFP kwamba katika mifano kadhaa waliposhambuliwa, polisi haikuitikia wito wao wa kuomba msaada. Sachim Sharma, Muhindu kwa dini yake, alisema kuwa ameshindwa kutoka nje "kwa sababu niliogopa kundi la watu lingelikuja nyumbani, wangeturushia mawe, wangechoma moto gari zangu, wanaweza kufanya chochote," huku mwezake Naem Malik, ambaye ni Muislamu, akisema waliwaita olisi mara kadhaa "kutoka Chand Bagh, tukiwaambia kuwa watu wanapiga kelele za 'Atukuzwe Mungu Ram' na wanaingia majumba yetu, lakini polisi hawakutusaidia."
Miongoni mwa watu 200 waliojeruhiwa, sita kati yao wako kwenye hali mbaya sana, alisema mkurugenzi wa afya wa Delhi, Sunil Kumar.
Eneo ambalo machafuko hayo yametokezea ni mitaa ya mabanda ya wahamiaji masikini, ambao wengi wameshayakimbia wakihofia kuwa huenda ghasia zikaendelea tena leo.
Machafuko haya yamesadifiana na ziara ya masaa 36 ya Rais Donald Trump wa Marekani ambaye alikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu Modi mjini Delhi jana Jumanne, ingawa aliondoka kama ilivyopangwa bila ya ziara yake kuathiriwa na machafuko hayo.
Sheria mpya iliyozuwa machafuko haya inakosolewa kukidhi ajenda ya Modi ya kuigeuza India kuwa taifa la Wahindu pekee, huku akiwatenga raia milioni 200 ambao ni Waislamu.