Utoaji wa gesi za Kaboni umeongezeka 2018
6 Desemba 2018Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo ni mkusanyiko wa tafiti tatu kutoka mradi wa ulimwengu kuhusu gesi za kaboni, utoaji wa gesi ya ukaa duniani umeongezeka kwa asilimia 2.7 kati ya mwaka 2017 na 2018 baada ya kuwa kiwango cha chini kwa miaka kadhaa iliyopita.
Ripoti hiyo imetolewa wakati wanadiplomasia kutoka mataifa mbalimbali duniani wanakutana mjini Katowice nchini Poland kwa muda wa wiki mbili kwa mkutano wa mabadaliko ya tabianchi wa COP24.
Wawakilishi kutoka karibu nchi 200 wanajaribu kuweka mkakati wa kufikia malengo ya kupunguza kiwango cha uchafuzi kilichokubaliwa kwenye mkataba wa Paris wa mwaka 2015, lakini wanasayansi tayari wamesema viwango vipya vya uchafuzi vinamaanisha itakuwa vigumu kufikia baadhi ya malengo.
Mkataba wa Paris unaweka masharti ya mataifa kufanya kazi pamoja kudhibiti ongezeko la joto ulimwenguni kuwa kati ya nyuzi 1.5 hadi 2 kwa kipimo cha Selshesi ambacho ni kiwango cha joto kabla ya mapinduzi ya viwanda mwaka 1750.
Ahadi ni nyingi bila vitendo
Akizungumza kwenye mkutano wa COP24 mshauri wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika taasisi ya Greenpeace Jens Mattias Clausen amesema ripoti hiyo mpya imetoa mwanga zaidi kwa kile kinachojulikana kote duniani kuwa mabadiliko ya tabianchi ni kitisho cha wazi na ulimwengu lazima ufanye kazi haraka kupunguza viwango utoaji wa gesi ukaa
Akiwanyooshea kidole cha lawama wanasiasa ambao wamekuwa chanzo cha kile alichokiita mwendo wa konokono katika kupunguza matumizi ya nishati chafuzi, mwakilishi huyo wa Greenpeace amesema "Kuna wanasiasa wengi wanaosema mambo chungu nzima wanayotaka kufanya, na mipango lukuki ya siku za usoni na mikakati ya kila aina waliyonayo, lakini inapokuja vitendo, hatuoni chochote. Kwa hiyo kimsingi hicho ndiyo tunakiomba wafanye, mtu awe kiongozi na sio mwanasiasa tu”
Viwango vya uchafuzi vimechangiwa zaidi na matumizi makubwa ya makaa ya mawe, mafuta na gesi asilia na watafiti wameonya kuwa ongezeko la mahitaji ya nishati duniani linatishia mipango ya kupunguza utowaji wa gesi ya ukaa.
China na Marekani vinara wa utoaji gesi ukaa
Takwimu za mwaka 2017 zinaonesha mataifa yanayongoza kwa utoaji wa gesi ukaa ni China kwa asilimia 27, Marekani kwa asilimia 15, Mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya yanachangia kwa asilimia 10 na India viwango vya uchangiaji wake ni asilimia 7.
Baadhi ya wajumbe wanaoshiriki mkutano wa COP24 huko Poland wamesema kulikuwa na majadiliano magumu jana wakati nchi zinazoendelea zilipotaka kupata hakikisho kuwa ikiwa zitaweka ahadi ya kupunguza utoaji wa gesi ya ukaa nchini tajiri zitakuwa tayari kulipia gharama za athari kwenye chumi za mataifa hayo masikini.
Mwandishi : Rashid Chilumba/DPA/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu