1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Magufuli na vita vya mtu mmoja

5 Agosti 2016

Rais John Magufuli ameifanya Tanzania kuhisi kama mahala tofauti na ilipokuwa muda mfupi uliyopita, anasema Jenerali Ulimwengu katika tathmini yake ya miezi sita ya kwanza ya Rais Magufuli madarakani.

https://p.dw.com/p/1Jbyu
Rais wa Tanzania, John Magufuli
Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Novemba mwaka jana, Magufuli amlimrithi Jakaya Mrisho Kikwete kutoka chama kilekile cha CCM kilichoiongoza Tanzania tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1961, lakini Magufuli amekuwa akitenda kama vile alitokea upinzani kwa namna alivokuwa anapindua mambo mengi.

Kwa fadhaa ya wengi waliompigia kampeni katika uchaguzi wa mwaka jana, rais Magufuli ameonyesha mamlaka yake kwa kufanya yale aliyoahidi kuyafanya wakati wa kampeni, ikiwemo kuondoa rushwa na uzembe katika utumishi wa umma. Katika kutimiza ahadi yake, JPM kama anavyofahamika kwa kifupi, amewafuta au kuwasimamisha kazi, na kuwaweka chini ya uchunguzi maafisa kadhaa wanaodhaniwa kuwa wazembe kazini au kusaidia na kuendekeza vitendo vya rushwa.

Amewatimua haraka maafisa wa juu wa mamlaka ya kodi ya taifa hilo kuhusiana na ulegevu katika makusanyo ya kodi, amewabadili mabosi wa juu wa Bandari sugu isiyo na ufanisi ya Dar es Salaam kuhusiana na tuhuma za upotevu wa ushuru wa forodha na mapato mengine ya serikali, amewasafisha viongozi wa juu wa shirika la taifa la hifadhi ya jamii, amefichua maelfu ya wafanyakazi hewa waliokuwa kwenye orodha ya mishahara ya serikali, na ameweza kuwazindua usingizini watumishi wengi wa umma.

Ukweli ni kwamba mengi ambayo Magufuli amesifiwa kuyafanya ni mambo ya kawaida na yanayopaswa kufanywa na serikali yoyote iliyoko madarakani, masuala kama ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa kodi, lakini kwa muda mrefu wafanyabiashara wenye mahusiano na chama tawala wamekuwa wakipewa misamaha ya kodi, wengi wakichukuliwa kuwa wafadhili wakubwa wa kampeni za uchaguzi za chama tawala. Utawala wa rais Kikwete ulikuwa tayari kutoa misamaha ya kodi kwa wafadhili wa kampeni za chama hicho tawala.

JPM amejitanabahisha kama mtu mwenye lengo la kuweka mambo sawa na kuiondoa nchi katika hali ya utepetevu na mazoea ya uvuvi, na kwa hilo, amepata sifa nyingi nyumbani na hata nje ya nchi. Tofauti kabisa na mtangulizi wake, JPM amekuwa rais wa kukaa nyumbani zaidi, akikataa ziara za nje, ambazo mtangulizi wake alizipenda sana kiasi kwamba aligeuka shabaha ya mzaha wa waandishi wa tashtiti.

Jenerali Ulimwengu ni mwandishi wa habari kutoka Tanzania
Jenerali Ulimwengu ni mwandishi wa habari kutoka TanzaniaPicha: privat

Ziara ya kwanza kabisaa ya Mgufuli nje ya nchi akiwa rais ilikuwa katika nchi jirani ya Rwanda, ambayo rais wake Paul Kagame alisifu msimamo imara wa Magufuli na kuutaja kama nguvu mpya katika muktadha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa ujumla, rais huyo mpya anaonekana kupata alama za juu katika namna alivyojaribu kuwadhibiti maafisa wake kwa dozi imara ya nidhamu. Lakini hajakosa wakosoaji ndani na kimataifa. Baadhi wanakosoa namna ambavyo amekuwa akitekeleza majukumu yake, akitoa maagizo ya papo kwa papo na kutoa maamuzi ya haraka. Wanamtuhumu kwa madoido na kukosa muundo. Jarida la Economist lilipuuza mfumo wake na kumkosoa kwa kufanya maamuzi bila kutafakari.

Wapo pia wanaozungumzia kile kinachoonekana kama unyakuzi wa madaraka ya bunge kwa mfano, kubadilisha fedha zilizotengwa kwa ajili mambo makhsusi na kuzipeleka katika maeneo mengine ambayo rais anadhani ndiyo yanastahili zaidi. Kuna mgogoro unaofukuta kati ya mhimili wa utawala na bunge, ambapo bunge linadai linazibwa mdomo.

Wanaomkosoa wanahofu kuwa mtindo wa kiburi ambao JPM amekuwa akiutumia katika utekelezaji wa majukumu yake unaanza kujipenyeza hata kwa watumishi wa ngazi za chini katika wizara, mikoa na hata wilaya. Mawaziri na watendaji wa serikali za mikoa na wilaya wamekuwa wakimuiga rais kwa kutoa maamuzi ya papo kwa papo kuhusu masuala ambayo yanaweza kuwa nje ya mamlaka yao kisheria na kikatiba.

Miezi hii ya mwanzo iliyopita imeonyesha taswira ya rais mwanaharakati ambaye huenda amekiuka baadhi ya sheria za msingi katika kufanya kile anachoamini kuwa kizuri kwa taifa. Miezi ijayo itaamuwa iwapo Magufuli ataitikia wito unaotolewa kwake kutekeleza majukumu yake kwa kushauriana na kuheshimu utawala wa sheria, au iwapo ataendelea na kile kinachoonekana kama vita vyake vya mtu mmoja dhidi ya nguvu zinazoweza kuwa imara zaidi yake.

Mwandishi: Jenerali Ulimwengu

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Saumu Yusuf