1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa kijeshi Myanmar wanyonga wanaharakati wanne

25 Julai 2022

Utawala wa kijeshi nchini Myanmar, umesema umewaua wanaharakati wanne wa demokrasia wanaotuhumiwa kusaidia katika kutekeleza matendo ya kigaidi. Tukio hilo imelaumiwa vikali kutoka kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/4EcDf
Min Aung Hlaing
Picha: Sefa Karacan/AA/picture alliance

Wakihukumiwa kifo  katika kesi za faragha mnamo mwezi Januari na Aprili, wanaume hao walishutumiwa kwa kusaidia vuguvugu la upinzani kupambana na jeshi lililotwaa madaraka kupitia mapinduzi mwaka jana na kuanzisha msako wa umwagaji damu dhidi ya wapinzani wake.

Gazeti la the Global New Light of Myanmar limeripoti kuwa miongoni mwa wale waliouawa ni mwanaharakati wa demokrasia Kyaw Min Yu waumri wa miaka 53 almaarufu Jimmy, Phyo Zeya Thaw, aliyekuwa mwanasheria na msanii, Hla Myo Aung na Aung Thura Zaw.

Soma pia: UN yaliambia jeshi la Myanmar liwache kuwauwa waandamanaji

Kyaw Min Yu na Phyo Zeya Thaw rafiki wa muda mrefu wa kiongozi aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi, walishindwa katika rufaa dhidi ya hukumu zao mnamo mwezi Juni.

Erwin Van Der Borght, mkurugenzi wa kanda wa shirika la haki la Amnesty International amesema mauaji hayo ni sawa na mauaji ya kiholela na ni mifano mingine ya rekodi ya ukandamizaji wa haki za binadamu ya Myanmar.

Bildkombo | Kyaw Min Yu und Phyo Zeya Thaw
Kyaw Min Yu na Phyo Zeya Thaw - Wanaharakati waliouawaPicha: AP/picture alliance

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Myanmar (NUG), iliyopigwa marufuku na uongozi wa kijeshi nchini humo, imetoa wito wa hatua za kimataifa dhidi ya jeshi hilo.

Shirika la reuters limeripoti kuwa Msemaji wa ofisi ya NUG Kyaw Zaw, amesema kuwa jamii ya kimataifa lazima iuadhibu utawala huo wa kijeshi kwa ukatili wake.

Soma pia: Myanamar: Jeshi limetangaza hali ya dharura na kuchukua madaraka

Huku hayo yakijiri, Ufaransa imelaani mauaji hayo na kuyataja kuwa kupindukia kwa ukandamizaji wa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.

Taarifa kutoa kwa wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa, imesema kuwa ijapokuwa hakuna mauaji yaliofanyika katika taifa hilo kwa zaidi ya miaka 30, mauaji ya aina hii yanachangia kupindukia kwa ukandamizaji wa utawala wa kijeshi na awamu nyingine katika kuongezeka kwa ukatili uliofanywa na utawala wa jeshi la Burma tangu mapinduzi ya kijeshi.

Wakati huo huo, Marekani pia imelaani mauaji hayo na kutoa wito kwa utawala wa nchi hiyo kuacha ghasia mara moja na kuwaachia huru wale waliozuiwa kinyume cha sheria .