Utafiti waonyesha kuwa Wamarekani vijana hawajui Holocaust
17 Septemba 2020Utafiti huo uliodhaminiwa na tasisi ya Kiyahudi ya Claims Conference umegundua kuwa takriban theluthi mbili ya walioulizwa hawakujua kwamba Wayahudi milioni sita waliangamizwa na utawala wa Wanazi katika mauaji ya Holocaust na asilimia 36 walijibu kwamba Wayahudi waliouawa ni milioni mbili au wachache zaidi ndiyo waliuawa.
Ripoti ya uchunguzi huo iliyotolewa siku ya Jumatano, inaonesha kuwa karibu nusu ya vijana hao walishindwa kutaja hata kambi moja kati ya 40,000 zilizojengwa barani Ulaya kwa ajili ya Wayahudi wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Aidha, wengine hawakujua kambi ya mateso na maangamizi ya Auschwitz-Birkenau ni kitu gani.
Rais wa taasisi hiyo, Gideon Taylor amesema matokeo hayo yanatisha na yanasikitisha. Amesema uchunguzi huo unasisitiza ni kwa nini hatua zinapaswa zichukuliwe sasa, wakati walionusurika na mauaji ya Holocaust bado wako hai kuhakikisha hadithi zao zinasikika. Kwa mujibu wa Taylor ambaye tasisi yake inajadiliana kuhusu fidia kwa walionusurika na mauaji hayo, hili linapaswa kuwa kama kengele ya kuwaamsha watu wote na kama mpango ambao unapaswa kushughulikiwa na maafisa wa serikali.
Viwango vya ufahamu
Utafiti huo umedhihirisha kuwa jiji la New York lilikuwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliodhani kuwa Wayahudi wanahusika na mauaji ya Holocaust, kwa karibu asilimia 20. Ripoti hiyo imegundua kwamba Wisconsin ilipata alama za juu zaidi kuhusu ufahamu wa mauaji ya Holocaust, huku Arkansas ikiwa imeshika nafasi ya chini kabisa, huku chini ya asilimia 17 ya watu waliohojiwa wakikidhi vigezo vya msingi vya uelewa wa kawaida.
''Alama ya uelewa'' ilihesabiwa kwa kutumia asilimia ya vijana ambao wamesikia kabisa kuhusu mauaji ya Holocaust, wanaweza angalau kuitaja kambi moja ya mateso, kambi ya maangamizi na wanajua kwamba Wayahudi milioni sita waliuawa katika mauaji ya Holocaust. Takriban theluthi mbili ya waliohojiwa waliashiria kwamba wanaamini mauaji kama ya Holocaust yanaweza kutokea tena.
Wakati huo huo, kiasi cha nusu ya vijana waliohojiwa wamekiri kusoma taarifa za kupotosha kwenye mitandao au taarifa za kuyapinga mauaji hayo ya Holocaust na karibu theluthi moja wameona alama za Wanazi kwenye mitandao yao ya kijamii au kwenye jamii zao.
Makamu wa rais wa taasisi ya Claims Conference, Greg Schneider anasema sio tu kwamba ukosefu wa ufahamu kuhusu mauaji ya Holocaust ambao unasikitisha, lakini pia idadi ya vijana waliozaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 na katikati mwa miaka ya 1990 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000 pamoja na kizazi cha baada ya hicho maarufu kama Gen Z ambao wameshuhudia watu wakiyapinga mauaji ya Holocaust kwenye mitandao ya kijamii.
Schneider anakiri kuwa ni wazi jamii inapaswa kupambana na upotoshaji huo wa historia na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha mitandao mikubwa ya kijamii inazuia kuruhusu taarifa kama hizo kwenye majukwaa yao. Takwimu hizi zimekusanywa kutokana na mahojiano waliyofanyiwa watu 2000 katika kila jimbo, kati ya vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 30. Waliohojiwa walichaguliwa bila mpangilio.
(DW https://bit.ly/3iFMbnt)