1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti wa Yale: Vikwazo vyaathiri uchumi wa Urusi

29 Julai 2022

Watafiti katika Chuo Kikuu cha Yale nchini Marekani wanasema uchumi wa Urusi unakabiliwa na uharibu mkubwa kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi, licha ya Moscow kupuuzia athari hizo

https://p.dw.com/p/4Es7l
Zentralbank von Russland
Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Waandishi wa ripoti hiyo wanadai kuwa kazi yao inatilia mashaka madai ya Moscow kuwa uchumi wake bado uko imara na kuwa nchi za Magharibi zinaumia Zaidi kupitia kile kinatajiwa kuwa ni "vita vya kuzorota uchumi.”

Soma pia: Gesi ya Urusi yazidi kupungua kuingia Ulaya

Utafiti huo wasemaje?

Timu ya watalaamu wa Yale ilitumia data ya watumiaji bidhaa na takwimu kutoka washirika wa kimataifa wa kibiashara na usafirishaji bidhaa wa Urusi, kupima shughuli za kiuchumi miezi mitano baada ya Moscow kuanzisha uvamizi wake nchini Ukraine.

EU yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi vikiwemo vya mafuta

Waligundua kuwa msimamo wa Urusi kama muuzaji wa bidhaa ng'ambo umeyeyushwa kabisa, baada ya kulazimika kugeuka kutoka kwa masoko yake makuu barani Ulaya kuelekea Asia.

Utafiti huo unasema uingizaji wa bidhaa nchini Urusi umeporomoka tangu vita vilipoanza, na nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa za kununua pembejeo, vipuri na teknolojia.

Timu hiyo iligundua kuwa uzalishaji wa ndani wa Urusi umekwama kabisa na haina uwezo wa kujaza nafasi za biashara zilizoanguka, bidhaa na vipaji. Watayarishaji wa ripoti hiyo wanasema hali hiyo imesababisha kupanda kwa bei za bidhaa na hasira ya watumiaji.

Russland | Güterzüge in Kaliningrad
Nchi zaMagharibi zimeiwekea Urusi vikwazoPicha: Vitaly Nevar/REUTERS

Huku kukiwa na karibu kampuni 1,000 za kimataifa zilizofunga milango yao nchini humo, Urusi imepoteza kampuni ambazo zinawakilisha karibu asilimia 40 ya patojumla la ndani kwa mujibu wa utafiti huo.

Soma pia: Serikali za Umoja wa Ulaya zakubaliana kuhusu mgawo wa gesi asilia

Ripoti hiyo imesema Putin anaingilia kati kwa kutumia njia isiyo endelevu ya kifedha ili kuficha mapungufu ya muundo wa kiuchumi.

Iliongeza kuwa bajeti ya serikali ya Urusi imetumbukia katika nakisi kwa mara ya kwanza na fedha za Kremlin zipo katika hali ngumu mno kuliko inavyoeleweka kawaida.

Soma pia: Ukraine yataka Urusi iwekewe vikwazo zaidi

Wakati huo huo, watafiti hao wamesema masoko ya kifedha ya Urusi – wakiweka jicho kwa utabiri wa usoni – ndio yanayofanya vibaya Zaidi ulimwenguni, hali inayopunguza uwezo wa kuvutia uwekezaji mpya wa kuufufua uchumi.

Takwimu zinazowafaa wao

"Tangu uvamizi huo, takwimu za kiuchumi za Kremil zimekuwa za kuchaguliwa, kwa kutoa maeneo ambayo hayaonekana kuwa mazuri kwao na kuchapisha tu yanayowafaa” unasema utafiti huo.

Ungarn Szazhalombatta | Druschba-Pipeline
Urusi imewekewa vikwazo vya mafutaPicha: Attila Kiskbenedek/AFP/Getty Imgaes

Takwimu mpya za uzalishaji wa viwanda wa Urusi kwa mwezi Juni zinaonyesha kuwa iliathirika pakubwa katika sekta nyingi ikilinganishwa na mwaka jana. Kwa magari, uzalishaji ulipungua kwa asilimia 89 wakati kwa nyaya za mawasiliano ulishuka kwa karibu asilimia 80.

Nini kinachofuata kwa uchumi wa Urusi?

Waandishi wa utafiti wa Yale walisema Urusi haina mbinu ya kujiondoa katika janga hilo la kiuchumi kama washirika wa Magharibi wataendelea kuungana kuhusu vikwazo.

Utafiti tofauti wa Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama uliochapishwa Juni pia unaashiria kuwa uchumi wa Urusi upo kwenye misukosuko mingi, licha ya kustahimili siki za mwanzo za kutangazwa vikwazo.

"Athari za vikwazo ndio zimeanza tu kushuhudiwa: matatizo ya uzalishaji na usambazaji yanaongezeka na mahitaji yanapungua kwa kasi.” "katika kipindi kirefu, uchumi wa Urusi utadorora Zaidi wakati kwa kiasi fulani ukiachana na biashara ya kimataifa.” Ilisema ripoti hiyo.