1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishwaji mapigano waheshimiwa Syria

13 Septemba 2016

Hali ya utulivu inaendelea kote nchini Syria, mnamo siku ya kwanza ya usitishwaji wa mapigano utokanao na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Urusi Ijumaa iliyopita.

https://p.dw.com/p/1K16J
Utulivu unaripotiwa katika maeneo yote ya Syria
Utulivu unaripotiwa katika maeneo yote ya SyriaPicha: Getty Images/AFP/M. Abazeed

Kuanzia jana jioni, hakuna milio ya risasi inayosikika nchini Syria, na Wasyria waliitumia ahueni hiyo kujimwaga mitaani, kusherehekea sikukuu ya Eid el-Adh'ha. Waandishi wa habari wa shirika la AFP wanasema wanashuhudia hali ya utulivu katika maeneo yote ya nchi, yawe yale yanayodhibitiwa na serikali, au yaliyo chini ya waasi. Shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria likiwa na makao yake nchini Uingereza, pia limethibitisha hali hiyo.

Kinachosubiriwa ni hatua ya pili ya makubaliano kati ya Marekani na Urusi, yaani usambazwaji wa misaada ya kiutu, inayosubiriwa kwa shauku kubwa katika baadhi ya maeneo.

Bado mapema kushangiria

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ambaye alihusika katika kuyafikia makubaliano hayo amewaambia waandishi wa habari mjini Washington, kwamba bado ni mapema kushangiria mafanikio ya mpango huo wa usitishaji mapigano.

Mpango wa usitishwaji mapigano uliafikiwa na mawaziri wa Mambo ya nje wa Marekani na Urusi, John Kerry na Sergei Lavrov
Mpango wa usitishwaji mapigano uliafikiwa na mawaziri wa Mambo ya nje wa Marekani na Urusi, John Kerry na Sergei LavrovPicha: Reuters/M. Trezzini

''Tutafanya tathmini ya mafanikio ya mpango huo siku baada ya nyingine, kuangalia tulipofika, lakini leo bila shaka ni mapema sana kufanya hivyo, kwa sababu tunazungumzia saa kadhaa tu za utulivu'' Amesema Kerry.

John Kerry amesema pamoja na changamoto nyingi zinazoukabili mpango huo ulioafikiwa baina yake na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ipo nafasi kubwa ya mpango huo kufanikiwa, na amewataka wadau wote kuunga mkono, akisema unaweza kuwa fursa ya mwisho ya kuinusuru Syria iliyoungana.

Wengi wana mashaka hali hii itadumu

Lakini wahusika wote hawana matumaini kama hayo ya John Kerry. Mwanaharakati wa upinzani, Nayef Mustafa, aliyeko katika mkoa wa Idlib ambako watu 13 waliuawa katika mashambulizi ya anga jana, amesema ingawa usiku wa kuamkia leo umekuwa kimya na kufurahiwa na kila mtu, wengi wanaamini hali hii itamalizika na sikukuu ya Iddi, na kwamba haitadumu kwa muda mrefu.

Wasyria wengi hawaamini kama utulivu huu utadumu kwa muda mrefu
Wasyria wengi hawaamini kama utulivu huu utadumu kwa muda mrefuPicha: Getty Images/AFP/O. H. Kadour

Mpango huo wa kusitisha mapigano, ambao utakuwa ukianza upya kila baada ya masaa 48, ni juhudi za hivi karibuni kabisa za kujaribu kumaliza mzozo wa Syria uliodumu kwa miaka mitano na kuuwa watu zaidi ya 290,000. Mipango yote ya awali iliambulia patupu.

Wakati hayo yakiarifiwa, shirika la habari la Syria, SANA, limeripoti kuwa Syria imezidungua ndege mbili za Israel, ikiwemo moja isiyoendeshwa na rubani, katika upande wa Syria wa milima ya Golan. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kitendo hicho kilikuwa ulipizaji kisasi wa shambulizi la Israel kwenye kambi ya wanaanga wa Syria ya Qunaitra kusini mwa Syria. Israel imekanusha mara moja ripoti hiyo, ikisema hakuna ndege yake hata moja iliyohujumiwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef