1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishwaji mapigano waanza kutekelezwa Syria

27 Februari 2016

Mizinga imesita kurindima nchini Syria halikadhalika mashambulizi ya anga ya Urusi wakati usitishaji wa uhasama ukianza kutekelezwa kwa siku ya kwanza Jumamosi (27.02.2016).

https://p.dw.com/p/1I3Ts
Wananchi wa Syria wakiota jua mjini Damascus na kusubiri kwa hamu usitishaji wa mapigano. (25.02.2016)
Wananchi wa Syria wakiota jua mjini Damascus na kusubiri kwa hamu usitishaji wa mapigano. (25.02.2016)Picha: picture alliance/Photoshot

Chini ya makubaliano kati ya Marekani na Urusi yaliyokubaliwa na serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria na maadui zake wengi,mapigano yanapaswa kusitishwa ili kutowa nafasi kwa misaada kufikishwa kwa raia na ili mazungumzo yaanze ya kukomesha vita vya nchi hiyo ambavyo vimeuwa zaidi ya watu 250,000 na kuwapotezea makazi wengine milioni 11.

Urusi imesema inakusudia kuendelea kufanya mashambulizi katika maeneo yanayoshikiliwa na wapiganaji wa misimamo mikali wa Kiislamu ambao hawahusiki na suluhu hiyo lakini imesema itasitisha safari zake zote juu ya anga ya Syria katika siku ya kwanza ya suluhu hiyo ili kuhakikisha hakuna makosa katika shabaha zake za mashambulizi.

Waasi wameelezea kuwepo kwa ukiukaji wa suluhu wa mara kwa mara unaofanywa na serikali na kamanda mmoja ameonya kwamba iwapo ukiukaji huo hautokaguliwa unaweza kupelekea kusambaratika kwa makubaliano hayo.

Vyombo vya habari vya taifa vimeelezea kuwepo kwa mashambulizi ya roketi karibu na Damascus yaliofanywa na kundi la Dola la Kiislamu.Lakini kwa jumla kiwango cha mashambuliz kimepunguwa sana.

Matumaini ya amani

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mastura amesema katika mkutano na waandishi wa habari usiku wa manane mjini Geneva kwamba " Tuombe makubaliano hayo yataweza kufanya kazi kwa sababu kusema kweli hii ni fursa bora kabisa ambayo wanaweza kufikiria watu wa Syria wameweza kuwa nayo katika kipindi cha miaka mitano iliopita,kuona kitu fulani kizuri na kutaraji kitahusiana na amani."

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura.Picha: Reuters/P. Albouy

Amesema anatarajia kutakuwepo na ukiukaji wa makubaliano hayo mara kwa mara lakini ametowa wito kwa wahusika kuchukuwa hatua za kujizuwiya na kudhibiti kupamba moto kwa mzozo huo.

Makubaliano hayo ni ya kwanza ya aina yake kujaribiwa katika kipindi cha miaka minne na iwapo yataweza kufanya kazi yatakuwa makubaliano yenye mafanikio makubwa kabisa ya suluhu kuwahi kushuhudiwa hadi sasa katika vita hivyo vya miaka minne.

Makundi ya itikadi kali

Makubaliano hayo hayajumuishi makundi yenye nguvu ya wapiganaji wa jihadi kama vile kundi la Dola la Kiislamu na Nusra Front ambalo ni tawi la Al Qaeda nchini Syria. Kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika na shambulio la kujitolea muhanga la mripuko wa gari katika jimbo la Hama. Kundi la Nusra limetowa wito wa kuongezwa mashambulizi maradufu.

Wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria.
Wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria.Picha: picture-alliance/AP Photo

Urusi na serikali ya Syria zinasema zitaendelea kupambana na makundi hayo na waasi wengine wanasema wana hofu wanaweza kutumia kisingizio hicho kuwashambuia wao.

Usitishaji huu wa mapigano ni hitimisho la juhudi za kidiplomasia ambazo zimezingatia kubadilika kwa medani ya mapambano tokea Urusi ijiunge katika vita hivyo hapo mwezi wa Septemba kwa mashambuzi ya anga kumsaidia Assad.Kuingilia kwa Urusi kumefuta kabisa matumaini waliokuwa nayo maadui zake Assad kwa miaka mitano yakishajiishwa na mataifa ya Kiarabu na yale ya magharibi ya kumn'gowa kwa kutumia nguvu.

Vikosi vya serikali vikisaidiwa na mashambulizi ya anga ya Urusi vimesonga mbele katika wiki za hivi karibuni na kuukaribia mji wa Allepo ambao ndio uliokuwa mji mkubwa kabisa nchini Syria kabla ya vita.

Marekani imesema wakati umefika kwa Urusi kuonyesha kwamba iko makini kuhusu usitishaji wa mapigano kwa kuheshimu ahadi zake za kutoshambulia makundi ya Syria ya msimamo wa wastani ambayo ni sehemu ya upinzani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Ssessanga, Iddi Ismail