1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishwaji mapigano kujumuisha Aleppo

Admin.WagnerD3 Mei 2016

Urusi imesema inatumai usitishaji mpya wa mapigano unaweza kutangazwa wakati wowote ule kuanzia sasa kwa mji wenye mapigano makali wa Allepo nchini Syria ambapo mapigano mapya yamesababisha vifo vya watu 16.

https://p.dw.com/p/1IhIP
Picha: Reuters/A. Ismail

Urusi imesema inatumai usitishaji mpya wa mapigano unaweza kutangazwa wakati wowote ule kuanzia sasa kwa mji wenye mapigano makali wa Allepo nchini Syria ambapo mapigano mapya yamesababisha vifo vya watu 16 likiwemo shambulio la roketi katika hospitali ya wazazi.

Wakati mji huo ukikumbwa na mapigano makali kabisa kuwahi kushuhudiwa katika siku za hivi karibuni waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergey Lavrov amesema juhudi ziko mbioni kufanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano na kwamba katika kipindi cha usoni yumkini masaa machache yajayo uamuzi huo ukatangazwa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura waziri huyo wa mambo ya nje wa Urusi pia amezungumzia azma ya Urusi na Marekani kuanzisha kituo cha kufuatilia kwa haraka ukiukaji wa mapigano nchini Syria.

Lavrov amesema "Mawaziri wa ulinzi wa nchi zote mbili wana utaratibu wa kuwasiliana kila siku na mawasiliano hayo ambayo hivi sasa yanafayika kwa kupitia kiungo cha video yanageuka kuwa mawasiliano ya moja kwa moja kwa kuanzisha siku zinazokuja huko Geneva kituo cha kufuatilia kwa haraka ukiukaji kwa usistishwaji wa mapigano nchini Syria."

Shinikizo la kusitishwa mapigano

Wiki hii mataifa yenye nguvu duniani yamekuwa yakishinikiza kwa pamoja kusitishwa kwa mapigano huko Allepo na kuyanusuru makubaliano ya kusitisha mapigano yaliofikiwa mwishoni mwa mwezi wa Februari.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov akikutana na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura mjini Moscow. (03.05.2016)
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov akikutana na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura mjini Moscow. (03.05.2016)Picha: Reuters/S.Karpukhin

Makubaliano hayo ya suluhu kati ya utawala wa Rais Bashar al- Assad wa Syria na waasi yalizusha matumaini ya hatimae kufanikiwa kwa juhudi za kuutauwa mzozo huo wa miaka mitano nchini Syria.Lakini makubaliano hayo yanaonekana kusambaratika kutokana na kuanza tena kwa mapambano hususan Aleppo.

Kuibuka upya huko mapigano kulikoanza hapo terehe 22 Aprili kumegharimu maisha ya zaidi ya watu 270 katika mji huo wa kaskazini uliogawika na kudhoofisha juhudi za kufufuwa mazungumzo ya amani.

Mei mwezi muhimu kwa Syria

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi mjini Moscow amezungumzia muhimu wa mwezi wa Mei kwa Syria ambapo amekaririwa akisema:

Mwanamke aliejeruhiwa katika mapigano ya Aleppo nchini Syria.
Mwanamke aliejeruhiwa katika mapigano ya Aleppo nchini Syria.Picha: Reuters/A. Ismail

"Mei utakuwa mwezi muhimu kwa Syria na kwetu sisi sote. Iwapo kama tunavyotarajia kutakuwepo na thibitisho fulani kwamba hata Allepo itarudi kwenye usitishwaji wa uhasama ambapo kile tutakachotarajia baadae itakuwa ni kushinikiza kupatikana kwa misaada ya kibinadamu na kufanyika kwa mazungumzo baina ya Wasyria."

Baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry hapo jana mjini Geneva mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa akiwa Moscow amesema ni muhimu kwa usitishwaji wa mapigano kurudishwa tena kwenye mkondo wake.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman