Usafiri wa umma wakwamishwa na mgomo Uganda
24 Agosti 2023Mvutano kati ya halmashauri ya mji wa Kampala na wamiliki wa mabasi hayo ndicho chanzo cha mgomo huo, pande zote zikikataa kukubaliana kuhusu ada mpya kwa mabasi kuendesha shughuli zake kwenye vituo binafsi katikati ya mji.
Mamia ya abiria waliopanga kusafiri kwa basi kwenda sehemu mbalimbali za Uganda wamejikuta mashakani kufuatia mgomo huo ambao ulianza ghafla bila ilani yoyote. Kulingana na wadau katika usafiri huo, si haki kwa halmashauri ya mji wa Kampala, KCCA, kuwatoza ada mpya za hadi shilingi milioni mbili laki nne kwa kila basi kila mwaka ili hali wao hulipa kodi kwa wamiliki wa vituo binafsi.
Ada ya milioni tatu kwa mwaka kwa kila basi
Kinacholeta kero zaidi ni mgomo huu kufanyika wakati wanafunzi wakirudi nyumbani kwa likizo. Abiria wengi wamekwama kwani hawawezi kulipa nauli kwa magari ya matatu ambayo yamepandisha nauli hizo maradufu kutokana na mahitaji mkubwa ya abiria.
Kulingana na waendeshaji wa biashara hiyo, kila basi hulipa kiasi cha shilingi milioni tatu za Uganda kila mwaka kama kodi na pia kupata leseni kuendesha shughuli zake. Pesa hizo ni kando na zile wanazolipa kukodi vituo binafsi wanakopakilia abiria. Ni kwa msingi huu ndipo wanashangaa kwa nini serikali isiingilie kati ikifahamu kuwa wao hutoa huduma muhimu kwa raia wa kawaida ikiwemo wafany biashara ndogondogo wanaotumia mabasi hayo kwa uchukuzi wa bidhaa zao.
Kwa upande wake msemaji wa Halmashauri ya mji wa Kampala KCCA Simon Kasyate amesisitiza kuwa makampuni hayo hayafai kulalamikia ada hiyo mpya kwani ni sehemu ndogo tu ya kipato chao kwa kila safari wanayofanya.
Mashauriano ya kutafuta suluhu yaendelea
Wizara ya elimu imelazimika kuingilia kati suala hilo na kuihimiza ile ya uchukuzi kushughulikia suala hilo kwa dharura kwani huu ni wakati ambapo wanafunzi wanasafiri. Wasipotatua suala hilo wanafunzi wengi watatatizika kufika makwao.
Mashauriano yamekuwa yakiendelea ili kutafutia suala hilo ufumbuzi, mabasi yarejelee huduma hizo bila kufungiwa. Siku ya Jumatatu, askari wa halmashauri ya KCCA walifungia mabasi yote kwenye vituo.
Tangu wakati huo, wafanyakazi wa mabasi ambao wengi ni vibarua wanaosaka riziki ya kila siku wamedumu katika dhiki na mashaka.