Urusi yawekewa vikwazo vipya na Umoja wa Ulaya
22 Februari 2021Watawala wakijeshi nchini Myanmar wamepewa onyo leo na Umoja wa Ulaya kwamba wajiandae kuwekewa vikwazo. Mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo kupitia mkutano wao mjini Brussels pia wamepitisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi.
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 27 za Umoja wa Ulaya katika mkutano wao wamejadiliana masuala mbali mbali na baadhi kuyapitishia uamuzi. Mawaziri hao pia wameungana kwa njia ya video na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken aliyesema nchi yake itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wanaochochea vurugu kwa wananchi wa Myanmar. Muda mfupi kabla ya mkutano huo mawaziri hao walitowa taarifa ya pamoja kuhusu Myanmar iliyosema kwamba Umoja huo unajiandaa kuchukua hatua kali zitakazowalenga waliohusika moja kwa moja na mapinduzi ya kijeshi pamoja na maslahi yao ya kiuchumi.Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas alisema
"Hatupo tayari kuendelea kutazama kinachoendelea Myanmar.Tutatumia njia zote za kidiplomasia zilizopo kuzuia matumizi ya nguvu na machafuko Myanamar lakini sambamba na hayo pia ikiwa hatutofanikiwa kuzuia machafuko,tutaangalia hatua ya kuchukua na kujiandaa kuweka vikwazo dhidi ya utawala wa kijeshi nchini Myanmar kama hatua ya mwisho.''
Msimamo kuhusu Urusi
Muda mfupi uliopita imeelezwa kwamba wamekubaliana kupitisha vikwazo dhidi ya maafisa wa Urusi kuhusiana na kisa cha kufungwa jela kiongozi wa upinzani Alexei Navalny pamoja na kukandamizwa kwa wafuasi wake.Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Joseph Borrell ametowa mwito wa kuchukuliwa hatua yenye kuonesha mshikamano na dhamira ya kweli ya Umoja huo katika suala hilo la Urusi.
Borrel amesema ni wazi Urusi iko katika mwelekeo wa kufuata njia ya mapambano na Umoja huo wa Ulaya. Waziri wa mambo ya nje wa Romania Bogdan Aurescu awali alidokeza kwamba mawaziri wengi wanaohudhuria mkutano huo wanaunga mkono vikwazo vipya dhidi ya Urusi. Washirika wawili wa karibu wa Navalny walitowa mwito wa kupitishwa vikwazo vitakavyowalenga washirika wa karibu zaidi na rais Putin.
Pendekezo hilo la upande wa Navalny lilitolewa jana Jumapili katika mkutano waliofanya na mawaziri wanane wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya huko Brussels. Kutibuka huku kwa uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi kunakoshuhudiwa sasa kumezidishwa na kile kilichoshuhudiwa hivi karibuni katika ziara ya mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Josep Borrel huko Moscow ambapo Urusi ilitangaza kuwafukuza wanadiplomasia watatu wa Umoja huo pamoja na kukataa mazungumzo ya ushirikiano.
Lakini pia Umoja huo wa Ulaya katika mkutano wake wa leo umeigeukia Venezuela ambapo umepitisha vikwazo vinavyowalenga maafisa 19 zaidi wa nchi hiyo wanaotuhumiwa kuhujumu Demokrasia au haki za binadamu katika nchi hiyo ya Kusini mwa Amerika.