Urusi yawapokonya vibali waandishi habari wa DW Moscow
4 Februari 2022Urusi imechukua hatua hiyo wakati ikiamuru kufungwa kwa ofisi za DW mjini Moscow kuanzia Ijumaa saa tatu.
Shirika la DW limetaja hatua hiyo kuwa ya kupitiliza na kusema itachukua hatua za kisheria.
Awali, Urusi iliikosoa marufuku iliyotolewa na mamlaka za vyombo vya habari Ujerumani dhidi ya shirika lake la utangazaji Russia Today, ikisema ni shambulizi dhidi ya uhuru wa habari na wa kujieleza.
Waziri Annalena Baerbock akutana na Lavrov mjini Moscow
Shirika la usimamizi wa vyombo vya habari la Ujerumani MARBB, na Kamisheni ya Leseni na usimamizi wa taasi za habari ZAK, zilisema kwamba shirika Russia Today tawi la Ujerumani, haliwezi kurusha matangazo yake nchini Ujerumani kwa kutumia leseni ya Serbia.
Hatua ya Urusi imeshutumiwa na kulaaniwa pakubwa Ujerumani.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la DW Peter Limbough amesema uamuzi wa Urusi umepitiliza, na kwamba hata hivyo unaipa DW nguvu na dhamira ya kuripoti matukio nchini Urusi. Kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha DW, Limbourg amesema:
" Ni wazi Urusi imechukuwa hatua zilizopitiliza na wala hii siyo kisasi ikiwa unataka kuiona hivyo. Kwanza kabisa huwezi kuilinganisha RT Ujerumani na Deutsche Welle kwa sababu sisi ni shirika la utangazaji la umma na sio kituo cha serikali. Kwa upande mwingine tunapaswa kuhakisha kuwa waandishi wa habari wa Urusi wanaendelea kufanya kazi kwa uhuru nchini Ujerumani na wanaweza kuripoti chochote wanachotaka, na hii sivyo ilivyo kwa wenzetu, kwa hiyo inasikitisha sana kuona jinsi serikali ya Urusi ilivyojibu".
Limbourg ameongeza kwamba hata kama itabidi waandishi wa DW kuondoka nchini Urusi, shirika lake halitaacha kuripoti matukio yanayotokea Urusi.
Urusi yamkamata mkosoaji mwingine wa Kremlin
Hata hivyo, Limbourg amesema uamuzi huo ni pigo kwa waandishi habari wa DW walioko Urusi ambao wanapenda nchi hiyo na utamaduni wao.
Kulingana na Limbourg, uamuzi wa Urusi hauwezi kuwa ulipizaji kisasi ikizingatiwa waandishi habari wa RT wanaendelea na kazi yao nchini Ujerumani tofauti na wa DW ambao wamepokonywa vibali vyao vya kazi nchini Urusi.
Uamuzi wa Urusi unaathiri zaidi mahusiano ya mataifa hayo
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema uamuzi wa Urusi unazidi kuzorotesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Waziri wa utamaduni na habari wa Ujerumani Claudia Roth amekosoa uamuzi huo na kusema Urusi imechukua hatua isiyo sawa.
Urusi imesema itawawekea vikwazo pia maafisa waliohusika katika kuipiga marufuku utangazaji wa shirika lake RT, dhidi ya kuingia Urusi.
(DW)