Urusi yateka vijiji viwili Ukraine
29 Agosti 2024Ikizinukuu duru za wizara ya ulinzi, mashirika ya habari ya Urusi yamesema leo kuwa vijiji hivyo ni vya Stelmakhivka kwenye jimbo la Luhansk, na Mykolaivka kwenye jimbo la Donetsk.
Mapema asubuhi, uongozi wa jeshi la Ukraine ulisema kuwa vikosi vyake vilikuwa vikiyazuia mashambulizi kwenye eneo la Stelmakhivka.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Radoslaw Sikorski amesema Urusi haiko tayari kwa mazungumzo ya amani na Ukraine, kwa sababu inaendelea kuitaka Ukraine iachie sehemu kubwa ya eneo lake.
Akizungumza na shirika la habari la PAP, Sikorski amesema Urusi inataka kuendelea kuitawala Ukraine, na maadam ni hivyo, Ukraine haitokubali.
Alikuwa anajibu tangazo la Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky, aliyesema anataka kuwasilisha mpango wa amani kabla ya uchaguzi wa Marekani mwezi Novemba.