1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Allepo, Idlib na Hama zashambuliwa

2 Oktoba 2015

Ndege za kivita za Urusi, zimefanya mashambulizi mpya kwenye maeneo 18 yanayodaiwa kuwa ngome za kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1Ghcr
Mashambulizi yaliyofanywa na Urusi nchini Syria
Mashambulizi yaliyofanywa na Urusi nchini SyriaPicha: imago/ITAR-TASS

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi, imeeleza kuwa ndege za kivita za Urusi leo zimeshambulia vituo vya mawasiliano kwenye jimbo la Allepo pamoja na kambi ya mafunzo ya wanamgambo ya Idlib, huku kambi ya kwenye jimbo la Hama ikiwa imeharibiwa kabisa.

Mashambulizi hayo yanafanyika huku Urusi ikisema kuwa mashambulizi ya anga ya Syria yatafanyika kwa muda wa miezi mitatu hadi minne. Alexei Pushkov, Mwenyekiti wa kamati ya bunge la Urusi inayoshughulikia masuala ya kigeni amesema zaidi ya mashambulizi 2,500 ya anga yaliyofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani nchini Syria, yameshindwa kulisambaratisha kundi la Dola la Kiislamu, lakini operesheni za majeshi ya Urusi zitafanikiwa.

Kauli hiyo imetolewa wakati ambapo Rais Vladmir Putin wa Urusi ameelekea Ufaransa kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wenzake wa Ufaransa, Francois Hollande na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kuuzungumzia mzozo wa Syria.

Ama kwa upande mwingine, Uturuki pamoja na washirika wake katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani, wameitaka Urusi kuacha mara moja mashambulizi dhidi ya waasi wa Syria, na kujikita zaidi katika kupambana na wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu.

Waziri Sergei Lavrov na Rais Bashar al-Assad
Waziri Sergei Lavrov na Rais Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/dpa/Stringer/Ap/Pool

Wasiwasi kuhusu uvamizi wa kijeshi Syria

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Ufaransa, Ujerumani, Qatar, Saudi Arabia, Uturuki, Uingereza na Marekani, imeelezea wasiwasi wake kuhusu mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na Urusi, ikifafanua kwamba mashambulizi hayo ndiyo kwanza yanachochea zaidi siasa za misimamo mikali.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema mashambulizi ya anga ya Urusi yanawalenga magaidi na mapambano yao dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu hayapaswi kuwekewa masharti.

''Lengo ni ugaidi na hatumuungi mkono mtu yeyote ambaye anafanya mambo kinyume na watu wake. Sisi tunapambana na ugaidi. Tunayalenga maeneo yote yanayohusishwa na kundi la Dola la Kiislamu,'' alisema Lavrov

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank Walter-Steinmeier ameikosoa hatua ya Urusi kuivamia kijeshi Syria, huku akionya kuwa hakuna suluhisho la kijeshi katika mzozo wa Syria.

Waziri Frank-Walter Steinmeier
Waziri Frank-Walter SteinmeierPicha: AFP/Getty Images/D. Emmert

Akiuhutubia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mjini New York, Marekani, Steinmeier amesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa inahitaji kuhakikisha utawala wa kidekteta wa Rais Bashar al-Assad unamalizwa Syria. Amesema vita vya Syria vitamalizika iwapo nchi zote zitashirikiana kwa pamoja.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,APE, DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman