Urusi yasema shambulizi la droni Kremlin lazima lilipizwe
4 Mei 2023Haya yanajiri wakati Rais wa Ukraine Volodymyr zelenskiy akifanya ziara katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague, Uholanzi, kutafuta uungwaji mkono zaidi.
Akiwa amevalia fulana na suruale za khaki ambazo zimekuwa ndio utambulisho wake, Zelenskiy amekaribishwa katika mahakama hiyo ya The Hague na rais wake Jaji Piotr Hofmanski.
Rais huyo wa Ukraine ambaye mapema Alhamis alikutana na wabunge wa Uholanzi atafanya mkutano pia na Waziri Mkuu Mark Rutte na haya ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali.
Ukraine inataka kumuua Putin
Uholanzi imekuwa muungaji mkono mkubwa wa Ukraine huku mnamo Februari Rutte akisema haondoi uwezekano wa kuipa Ukraine msaada wa kijeshi bora tu usiitie Jumuiya ya Kujihami ya NATO katika mzozo na Urusi.
Ziara hii ya Zelenskiy ambayo haikutangazwa kabla, ya kukutana na maafisa wakuu wa mahakama ya ICC, ambayo imetoa waranti wa kukamatwa kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi, inajiri siku moja baada ya Moscow kuituhumu Kyiv kwa shambulizi la ndege isiyokuwa na rubani katika ikulu ya Kremlin.
Urusi imeituhumu Ukraine kwa kujaribu kumuua Putin na imesema shambulizi hilo ni lazima lilipizwe. Urusi vile vile imesema shambulizi hilo linaonyesha kuwa Ukraine haiko tayari kuumaliza mzozo huo katika meza ya mazungumzo. Ila Zelenskiy yeye amekanusha kuhusika kwa nchi yake na shambulizi hilo.
"Hana ushindi katika uwanja wa mapambano, jeshi la pili kwa ukubwa duniani limeshindwa. Hawawezi kuikalia Ukraine, tuliwazuia, na sasa anataka kutafuta uwezekano wowote wa kuwapa motisha wanajeshi wake kusonga mbele. Waliosalia ni hao wapiganaji wa Wagner tu ambao wanajumuisha wafungwa ambao watapigwa risasi na wenzao iwapo watarudi nyuma," alisema Zelenskiy.
Watu 23 wafariki dunia kutokana na mashambulizi
Haya yote yanafanyika wakati ambapo mapema Alhamis Urusi imefanya mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani nchini Ukraine, mashambulizi yaliyolenga jengo la chuo kikuu katika mji wa Bahari Nyeusi wa Odesa.
Hapo Jumatano mashambulizi ya Urusi yalisababisha vifo vya watu 23 ndani na karibu na mji wa kusini mwa Ukraine wa Kherson. Kulingana na gavana wa eneo hilo mashambulizi hayo yalifanywa katika duka moja la jumla, kituo cha treni na majengo ya makaazi.
Kwengineko Ukraine imesema mfumo wake wa ulinzi wa angani umezuia mashambulizi 18 kati ya 24 ya Urusi ya ndege zisizokuwa na rubani za kamikaze, zilizorushwa mapema leo.
Utawala wa mji wa Kyiv unasema makombora na droni zote zilizorushwa kuulenga mji huo mkuu kwa mara ya tatu katika kipindi cha siku nne, zimeharibiwa.
Chanzo: Reuters/AFPE