Urusi haitochunguza ajali ya ndege iliyomuua Prigozhin
30 Agosti 2023Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner Yevgeny Prigozhin, manaibu wake wawili na walinzi wanne walikuwa miongoni mwa abiria 10 waliokufa baada ya ndege iliyotengenezwa Brazil aina ya Embraer kuanguka kaskazini mwa mji mkuu wa Moscow wiki iliyopita.
Soma pia: Vipimo vya DNA vyathibitisha kifo cha Prigozhin
Kituo cha utafiti na usalama wa anga cha Brazil CENIPA, kwa maslahi ya kuboresha usafiri wa anga, kimeeleza utayari wao wa kujiunga na uchunguzi unaoongozwa na Urusi juu ya ajali hiyo, iwapo wangealikwa na Urusi na pia uchunguzi huo kufanyika chini ya sheria za kimataifa.
Mkuu huyo wa kundi la mamluki la Wagner amekufa miezi miwili tu baada ya kufanya uasi uliodumu kwa muda mfupi dhidi ya jeshi la Urusi na kutishia utawala wa Rais Vladimir Putin tangu alipoingia madarakani mnamo mwaka 1999.
Kremlin yakanusha kuhusika na ajali iliyomuua Prigozhin
Mamlaka ya anga ya Urusi haikulazimika kuridhia pendekezo la CENIPA japo baadhi ya wachunguzi wa zamani wanasema Urusi inafaa kukubali kushirikiana na Brazil.
Marekani na baadhi ya mataifa ya Magharibi yanashuku kwamba ikulu ya Kremlin imehusika moja kwa moja na ajali hiyo iliyotokea Agosti 23, iliyohusisha ndege aina ya Embraer Legacy 600 ambayo kwa kawaida ina rekodi nzuri ya usalama.
Kremlin hata hivyo imekanusha kuhusika kwa njia yoyote ile na ajali hiyo.
Prigozhin alikuwa mkosoaji mkubwa wa Moscow hasa juu ya uvamizi wake nchini Ukraine.
Wapiganaji wake wanapambana katika vita hivyo kwa niaba ya Urusi.
Soma pia: Putin ataka wapiganaji binafsi kula kiapo kwa taifa
Kulingana na shirika la usafiri wa anga la Umoja wa Mataifa lenye makao makuu yake mjini Montreal ICAO, ndege iliyombeba Prigozhin ilikuwa inatokea Moscow kuelekea St Petersburg, na kwa mujibu wa kanuni za usafiri inachukuliwa kama usafiri wa ndani kwa hivyo hakuna ulazima wa kutumika sheria za kimataifa kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.