Urusi yapeleka makombora Kaliningrad
7 Februari 2018Taarifa zinaeleza kuwa Urusi imepeleka kwenye eneo hilo mfumo wa makombora ya nyuklia unaojulikana kama Iskander. Akizungumza na waandishi habari mjini Moscow, msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dimitry Peskov amesema suala la kupeleka silaha au vikosi vya jeshi katika eneo lolote la Urusi ni uhuru na haki ya Shirikisho la Urusi. Amesisitiza kuwa Urusi haijawahi kumtishia mtu yeyote na kwamba haimtishi mtu na kwa kawaida Urusi ina haki yake na haipaswi kuwa sababu ya mtu yeyote kuwa na wasiwasi.
Hatua hiyo ya Urusi imekosolewa vikali na mataifa jirani pamoja na Jumuia ya Kujihami ya NATO. Kaliningrad ni eneo la Urusi katika Bahari ya Baltic na makombora hayo yatakuwa na uwezo wa kufika sehemu kubwa ya maeneo ya Poland, Lithuania, Latvia na Estonia ambazo ni nchi wanachama wa NATO.
Lithuania yatoa taarifa rasmi
Siku ya Jumatatu, Rais wa Lithuania, Dalia Grybauskaite alisema kuwa Urusi imepeleka makombora hayo Kaliningrad, eneo ambalo liko karibu na Lithuania. Rais huyo amesema hatua hiyo ni kitisho kwa Ulaya.
''Nataka kuwajulisha, labda kwa mara ya kwanza taarifa rasmi, kwamba ninavyozungumza hapa, mfumo wa makombora wa Iskander unapelekwa katika mkoa wa Kaliningrad. Hii kwa mara nyingine inaifanya hali hata kuwa mbaya zaidi kwa sababu Iskander katika eneo la Kaliningrad ni hatari kwa nusu ya miji mikuu ya Ulaya,'' alisema Grybauskaite.
Aidha, taarifa hizo zilielezwa pia na mbunge wa Urusi. Hata hivyo, Urusi haijathibitisha kuhusu madai hayo. Mara kwa mara Ikulu ya Urusi ilikuwa inasema itaweka mfumo huo wa makombora katika mkoa wa Kaliningrad ili kujikinga na makombora ya Marekani mashariki mwa Ulaya. Marekani imesema lengo la makombora hayo ni kukabiliana na mashambulizi ya makombora kutoka Iran. Hata hivyo, Urusi imesema makombora hayo yameelekezwa kwa Urusi.
Kupelekwa kwa makombora hayo karibu na maeneo ya NATO kunachukuliwa na baadhi ya wanachama wa jumuiya hiyo kama kitisho katika wakati ambapo mzozo unaongezeka kati ya Urusi na mataifa jirani ya Magharibi kutokana na hatua ya Urusi kuinyakua Rasi ya Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014.
Afisa mmoja wa NATO ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema kupelekwa kwa makombora ambayo yanaweza kubeba vichwa vya makombora ya nyuklia katika mipaka ya nchi wanachama wa NATO, hakusaidii kupunguza mvutano. Amesema wanaelewa kuwa Urusi imekuwa ikipeleka vifaa Kaliningrad kwa muda mrefu na wanatarajia kusikia zaidi kutoka kwa Urusi kuhusu yanayoendelea.
Hayo yanajiri wakati ambapo Marekani wiki iliyopita ilisema kuwa itaimarisha na kuongeza kiwango cha silaha zake za nyuklia. Wizara ya ulinzi ya Marekani ilitoa tathmini kuhusu kitisho cha nyuklia katika miongo ijayo kuhusu mpango ulioainisha wazi mkakati mpya wa utawala wa Rais Donald Trump wa kijeshi pamoja na kinyuklia.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, Reuters, http://bit.ly/2E3vPVs
Mhariri: Yusra Buwayhid