1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaishambulia Ukraine kwa madai ya kuanzisha uchokozi

10 Agosti 2024

Urusi imeshambulia maeneo matatu ya mpakani nchini Ukraine kujibu operesheni ya kijeshi iliyoanzishwa na Kiev siku nne zilizopita, operesheni inayosemekana kuwa kubwa zaidi tangu Urusi ianzishe uvamizi wake Ukraine.

https://p.dw.com/p/4jKJs
Russland | Region Kursk nach Ukrainischen Angriffen
Picha: Anatoliy Zhdanov/Kommersant/Sipa USA/picture alliance

Kamati ya kupambana na ugaidi ya Urusi imesema imeanzisha mashambulizi hayo katika maeneo ya Belgorod, Bryansk na Kursk, ili kuhakikisha usalama wa raia wake na kujaribu kudhibiti kitisho ilichokiita cha kigaidi kinachofanywa na adui yake.

Chini ya sheria ya Urusi vikosi vya usalama na wanajeshi hupewa mamlaka kamili ya dharura katika uwanja wa mapambano hasa katika matukio ya kupambana na ugaidi. 

Ukraine inaendeleza mashambulizi yake dhidi ya Urusi

Kamati hiyo imesema Ukraine imejaribu kuisambaratisha Urusi katika maeneo kadhaa ya taifa lake kwa kuwajeruhi raia na kuharibu baadhi ya majengo yake.

Hata hivyo Ukraine bado haijasema lolote juu ya operesheni hiyo inayosemekana kusababisha mauaji ya watu 66 wakiwemo watoto tisa nchini Urusi.