1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaionya UN dhidi ya uchunguzi wa ndege za Iran Ukraine

20 Oktoba 2022

Urusi imeuonya Umoja wa Mataifa kuachana na hatua ya kuchunguza kile kinachodaiwa mashambulizi ya ndege zinazorushwa bila ya rubani zilizotengenezwa Iran, ikiungana na serikali ya Iran kukanusha asili ya silaha hizo.

https://p.dw.com/p/4ISLa
Ukraine | russischer Drohnen-Angriff in Kiew
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Marekani, Ufaransa na Uingereza  kwa pamoja zilishiriki kikao cha ndani cha Baraza la Usalama kilichohusu madai ya Iran kuiuzia Urusi ndege hizo zisizo na rubani, ambazo wamezielezea kuwa ni ukiukaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa katika biashra ya silaha kwa Iran.

Umoja wa Ulaya na Marekani kwa pamoja wanasema wana ushahidi wa kutosha kwamba Iran ilisambaza ndege za aina ya Shahed-136, ndege zisizo na rubani za bei nafuu ambazo huripuka zikitua na zinadaiwa kusababisha vifo vya watu watano katika matukio ya Jumatatu iliyopita mjini Kyiv na kadhalika kwa uharibifu wa miundombinu ya raia.

Ukraine yajitenga kidiplomasia na Iran

Ukraine | russischer Drohnen-Angriff in Kiew
Polisi wa Ukraine akiishambulia ndege inayorushwa bila ya rubaniPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Ukraine, ambayo imefanya uamuzi wa kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na serikali ya Tehran, imesema jeshi lake limeziangusha ndege ya aina hizo zaidi ya 220 katika muda wa zaidi ya mwezi mmoja na na kumeonekana taswira zenye kuonesha mahusiano ya ndege hizo na Iran. Lakini mwandadiplomasia wa Urusi, Dmitry Polyanskiy alisema madai hayo hayana msingi wowote na ni nadharia ya njama tu.

Polyanskiy amenukuliwa akisema "Leo hii tumeshuhudia awamu nyingine ya kampeni ya upotoshaji kutoka katika Baraza la Usalama, inayofanywa na wajumbe wa mataifa ya Magharibi, katika suala la ndege zisizo na rubani zinazodaiwa kutumiwa na Urusi nchini Ukraine. Lengo la wenzetu hawa wa Magharibi liko wazi. Wanajaribu kuyashambulia maeneo mawili kwa wakati mmoja, na kubuni kisingizio bandia cha kuweka shinikizo kwa Urusi na Iran.

Vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya kwa Iran

Hata hivyo, hivi karibuni Umoja wa Ulaya umeridhia kuchukuliwa hatua mpya dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa taifa lenye kushikilia urais wa kupokezana wa umoja huo kwa sasa, Jamhuri ya Czech mataifa hayo yamekubaliana kuzuia mali za mtu mmoja mmoja na kampuni iliyohusika na usambazaji wa ndege zisizo na rubani na kadhalika inajiandaa kupanua wigo wa vikwazo kwa taasisi nne za Iran ambazo pia zimeguswa na vikwazo vya awali.

Soma zaidi: Putin atangaza sheria za kijeshi mikoa minne Ukraine

Katika hatua nyingine  Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema Rais Vladimir Putin anatumia nishati na njaa kama silaha za kivita, lakini ameshindwa kuutenganisha mshikamano wa mataifa ya Magharibi. Akiyazungumza hayo ndani ya bunge la Ujerumani, amesema taifa lake limejikomboa katika utemegezi wa gesi ya Urusi na kwa sasa lipo katika jitihada ya kufanikisha kushushwa kwa bei ya nishati ikiwemo pia kutafuta vyanzo vipya vya nishati kutoka katika mataifa mengine.

Vyanzo: AFP/RTR