1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yaionya Marekani dhidi ya kuingilia uchaguzi wake

11 Machi 2024

Shirika la ujasusi wa nje la Urusi SVR, limeishtumu Marekani kwa kujaribu kuingilia uchaguzi wake wa urais na kusema nchi hiyo pia ina mipango ya kuanzisha mashambulizi ya mtandaoni dhidi ya mfumo wa kupiga kura

https://p.dw.com/p/4dOqZ
Rais wa Urusi Vladimir Putin akitoa hotuba yake ya  mwaka kwa bunge la nchi hiyo mjini Moscow mnamo Februari 29, 2024
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Putin, ambaye ana matumaini ya kushinda uchaguzi huo wa urais utakaofanyika kuanzia Machi 15 hadi 17, ameyaonya mataifa ya Magharibi kwamba juhudi zozote za mataifa ya nje za kuingilia uchaguzi nchini Urusi zitachukuliwa kama kitendo cha uchokozi.

SVR inasema ina taarifa kuhusu madai yake dhidi ya Marekani

Shirika la habari la serikali ya Urusi, limelinukuu shirika la SVR likisema lina taarifa juu ya utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden kujipanga kuingilia uchaguzi huo wa Urusi.

SVR imesema Marekani inataka kufanya vigumu kuhesabu kura zitakazopigwa 

SVR imeendelea kusema kuwa utawala huo wa Biden kwa ushirikiano na wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano wa Marekani, umepanga kufanya mashambulizi hayo ambayo yatafanya kuwa vigumu kuhesabu kiasi kikubwa cha kura zitakazopigwa.

Hata hivyo, shirika hilo la ujasusi la SVR, halikutoa ushahidi wowote kuhusiana na madai hayo na pia hakukuwa na tamko la haraka kutoka Marekani.

Filamu ya Ukraine dhidi ya Urusi yashinda tuzo ya kimataifa ya Oscar

Rais  Zelensky, amepongeza hatua ya kutunukiwa tuzo ya kimataifa ya filamu ya Oscar kwa filamu moja inayohusu shambulio la Urusi katika mji wa Mariupol, na kusema imeonesha kile alichokiita ukweli kuhusu ugaidi wa Urusi.

Soma pia: Putin afanya ziara ya kushtukiza Mariupol na Crimea

Filamu hiyo kwa jina '' Siku 20 mjini Mariupol'' ilishinda tuzo ya filamu bora zaidi ya Oscar katika hafla iliyofanyika siku ya Jumapili mjini Los Angeles nchini Marekani.

Majengo yalioporomoka kutokana na mashambulizi ya Urusi mjini Mariupol nchini Ukraine mnamo Machi 16, 2023
Majengo yalioporomoka mjini Mariupol nchini UkrainePicha: AA/picture alliance

Filamu hiyo iliyoongozwa na mtengenezaji filamu wa Ukraine Mstyslav Chernov, inaonesha mapigano makali na mashambulizi mfululizo ya anga ya Urusi kutoka mji huo wa bandari ya Kusini mwa Ukraine katika siku za kwanza za uvamizi wa Urusi nchini humo mnamo mwaka 2022.

Mapema leo Ikulu ya Kremlin ilikataa kutoa maoni kuhusu ufanisi wa filamu hiyo.

Ikulu ya Kremlin yatetea matamshi ya papa Francis

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amesema leo kuwa Urusi inayachukulia matamshi tata ya kiongozi wa kanisa Katoliki dunia papa Francis sio kama wito kwa Ukraine kukubali kushindwa lakini kama wito wa mazungumzo.

Soma pia:Ukraine: Rais Volodymyr Zelensky asema diplomasia ndio njia pekee ya kuvimaliza vita

Peskov ameongeza kuwa mara nyingi Rais Putin ameelezea kuwa tayari kwa mazungumzo na kwamba hiyo ndio njia inayopendekezwa.

Kansela wa Ujerumani apinga matamshi ya papa Francis

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pia amepinga matamshi ya kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis. Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit amesema kuwa kansela Scholz  hakubaliana na matamshi ya papa Francis na kwamba Ukraine inajilinda dhidi ya mchokozi.

Mapema mwezi Februari katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha Uswisi, papa Francis alisema kuwa mhusika hodari ni yule anayefikiria kuhusu watu na mwenye ujasiri wa kuinua bendera nyeupe na kuinga kwenye majadiliano.