Urusi yadai kumuua kiongozi mkuu wa IS
16 Juni 2017Ikiwa madai ya Urusi yatathibitika kuwa kweli, basi mashambulizi ya ndege aina ya Sukhoi usiku wa tarehe 27 Mei karibu na mji wa Raqqa, yatakuwa yameyahitimisha maisha ya Baghdadi, mmoja wa watu waliokuwa wakitafutwa sana kutokana na dhima yake kwenye mauaji na mashambulizi ya kikatili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na jeshi la Urusi, siku hiyo viongozi 30 wa ngazi za juu wa kundi la IS walikuwa wanakutana kuzungumzi kujiondoa kwenye ngome yao hiyo, na mashambulizi hayo ya anga yaliangamiza maisha yao, pamoja na wapiganaji wao wapatao 300.
"Kutokana na taarifa ambazo zinachunguzwa kwa umakini kupitia vyanzo mbalimbali, kiongozi wa Daesh, Ibrahim Abu Bakr Al-Baghdadi pia alikuwepo kwenye mkutano huo na aliuawa," inasema taarifa hiyo, ikitumia jina la Kiarabu la IS, yaani Daesh.
Mashambulizi hayo yalifanyika kufuatia hakikisho la kuwepo kwa mkutano huo kupitia taarifa zilizokusanywa na ndege isiyo rubani. Miongoni mwa waliouawa ni amiri wa Raqqa na mkuu wa ujasusi wa Daesh, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Urusi, inayoongeza pia kuwa Marekani ilikuwa imefahamishwa na mapema juu ya kufanyika kwa mashambulizi hayo.
Marekani haina uhakika
Hata hivyo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani haujathibitisha kifo cha Baghdadi. Msemaji wa operesheni wa muungano huo, Kanali Ryan S. Dillon, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hawawezi kusema endapo taarifa ya Urusi ni ya kweli hadi sasa.
Baghdadi hajawahi kuonekana hadharani tangu ajitangazie ukhalifa mjini Mosul nchini Iraq, miaka mitatu iliyopita. Kundi lake linatambulika duniani kote kwa kuweka mfumo mkali wa Kiislamu na adhabu za kikatili, ikiwemo kupiga watu mawe, kuwakata vichwa na au viungo vyao vya mwili.
Mzaliwa huyo wa Iraq anayetafutwa sana amekuwa akivumishiwa kujeruhiwa ama kuuawa kwenye matukio kadhaa huko nyuma, kiasi cha kubatizwa jina la "mzuka", akiripotiwa kuwapo kwenye eneo la mpaka wa Syria na Iraq, lakini taarifa zake hazijawahi kuthibitishwa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman