Urusi yaadhimisha miaka 75 ya ushindi dhidi ya Wanazi
24 Juni 2020Rais Vladmir Putin ametoa matamshi hayo katika gwaride kubwa la wanajeshi kwenye Uwanja Mwekundu (Red square) mjini Moscow, katika sherehe ya kuadimisha miaka 75 tangu jeshi la Kisovieti maarufu kama ''Red army'' kuishinda Ujerumani iliokuwa chini ya utawala wa Wanazi katika Vita vikuu vya pili vya dunia.
''Ni vigumu hata kufikiria jinsi dunia ingekuwa kwa sasa ikiwa jeshi la Muungano wa Kisovieti halikujitolea kupigana na Wanazi,'' rais huyo amewambia maelfu ya wanajeshi waliokusanyika katika Uwanja Mwekundu huku akiongeza kuwa jeshi hilo lilizikomboa nchi za Ulaya kutoka kwa uvamizi, kukomesha mauaji ya Wayahudi pamoja na kuikomboa Ujerumani kutoka katika utawala wa Wanazi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, kiongozi huyo anatumia matamshi hayo yenye hisia za kizalendo katika kipindi muhimu kwake ambapo mnamo Juni 24 nchi hiyo itashiriki kura ya maoni kuhusu pendekezo la Putin la kufanya marekebisho ya katiba. Ikiwa marekebisho hayo yatafanyika huenda yatamwezesha kusalia madarakani hadi mwaka 2036.
Soma zaidi: Putin asema Warusi wengi wanamuunga mkono kubadilisha katiba
Awali, maadhimisho hayo yanayofanyika Mei 9 kila mwaka yalilazimika kuahirishwa kutokana na janga la virusi vya Corona. Ni hafla kubwa kuandaliwa na ikulu ya Kremlin tangu kulegezwa kwa vizuizi vya kudhibiti maambukizi ya COVID-19.
Hata hivyo, katika hotuba yake, Putin hakuzungmzia kuhusu janga hilo, baadhi ya wachambuzi wanasema rais huyo anataka kutoa fikra ili kusisitiza kauli yake mapema kwamba Urusi sasa imetoka katika hali hatari ya janga la COVID-19 licha ya kuwa nchi hiyo ni ya tatu duniani kwa idadi ya maambukizi mengi ya virusi vya Corona.
Katika muktadha huo pia rais wa Kyrgyzstan Sooronbai Jeenbekov ambaye alitarajiwa kuhudhuria sherehe hizo alikosekana baada ya wasaidizi wake wawili waliomsindikiza kupatikana na COVID-19 mara baada ya kuwasili mjini Moscow, ofisi ya rais imesema.
Maadhimisho hayo yalijumuisha wanajeshi 14,000 kutoka mataifa 13 ikiwemo China, India, Mongolia pamoja na Serbia huku Urusi ikitumia ukumbi huo kuonyesha zana zake za vita.
Katika utawala wake, rais Putin amekuwa akitumia mbinu ya kuusifu ushindi wa jeshi la Kisovieti katika vita vikuu vya pili vya dunia kufufua hisia za moyoni za uzalendo wa Warusi pamoja na kutafuta uungwaji mkono kwa serikali yake.
Vyanzo: AFP/Reuters/AP