Urusi kujenga kinu cha kwanza cha Nyuklia Misri
11 Desemba 2017Rais Vladmir Putin wa Urusi yuko Misri ambako ameshakutana na mwenyeji wake rais Abdel Fatah el sisi na kuzungumzia juu ya nchi hizo mbili kutanua ushirikiano zaidi. Putin amekwenda Misri baada ya kufanya ziara fupi ya kushtukiza nchini Syria alikotembelea kambi ya jeshi la wanaanga la Urusi.Akiwa Syria pia alikutana na rais Bashar al Assad.
Ziara ya rais Putin nchini Misri inaangaliwa kama ishara ya kuongezeka ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na hasa ikizingatiwa kwamba rais Abdel Fatah el sisi ameshakwenda Urusi mara tatu tangu alipomuondoa madarakani mtangulizi wake Muhammed Morsi mwaka 2013.Baada ya kuingia madarakani El Sissi ameingiza silaha zenye thamani ya mabilioni ya dolla kutoka Urusi zikiwemo ndege za kijeshi na helikopta za kufanya mashambulio.
Urusi nayo kwa upande wake mwezi uliopita iliidhinisha mkataba na Misri wa kuruhusu ndege zake kutumia kambi za kijeshi za Misri katika Mashariki ya kati.Leo hii viongozi hao wawili wametiliana saini mkataba wa Urusi kujenga kinu cha kwanza cha nyuklia nchini Misri kitakachojengwa katika eneo la Dabaa kwenye pwania ya bahari ya meditterrania.
Misri imekuwa ikiiunga mkono chini chini kujiingiza kwa Urusi nchini Syria katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.Kadhalika Urusi imesema iko tayari kusaini rasimu na Misri juu ya kuanzisha tena safari za ndege za moja kwa moja kutoka Moscow hadi Cairo wiki hii.
Ziara hii ya Putin imefuatia ziara yake ya ghafla huko nchini Syria ambako pia alikutana na rais Bashar al Assad na kutangaza kwamba Urusi inaondowa wanajeshi wake nchini humo akisema kwamba wameshafanikisha kwa pamoja na jeshi la Syria kile kilichotakiwa,ambacho ni kuwaangamiza magaidi.
''Ugaidi ni kitisho kote duniani na bado ni kitisho kikubwa.hata hivyo jukumu la kukabiliana na majambazi wenye silaha hapa syria,jukumu ambalo lilikuwa ni muhimu kulikamilisha kwa msaada mkubwa wa vikosi vya wanajeshi,kwa sehemu kubwa tumelikamilisha na tumelikamilisha barabara.Nawapongeza nyote.
Putin aliyazungumza hayo akiwa katika kambi ya jeshi la wanaanga la Urusi nchini Syria kambi ambayo imekuwa ikiendesha kazi muhimu katika kampeni ya nchi hiyo ya kushambulia kutokea angani tangu mwezi Septemba mwaka 2015 katika hatua ya kumuunga mkono rais Bashar Al Assad dhidi ya makundi ya waasi yanaoupinga utawala wake.Putin pia amesisitiza kwamba kikosi cha nchi yake kinaondoka kwa sehemu tu.
'' Tumeweka vituo viwili ambavyo vitaendelea kufanya kazi katika kipindi cha kudumu kwenye eneo la Tartous na hapa Hmeymim. Na endapo magaidi watajitokeza tena tutawashambulia kwa nguvu ambazo hawajawahi kuziona mwanzoni''
Ikumbukwe katika mgogoro huu wa Syria Misri kwa upande mwingine imekuwa ikiiinua sifa yake kwa kusimamia mazungumzo ya kusitisha vita kati ya serikali na makundi ya upinzani mazungumzo ambayo yamepata baraka zote za serikali ya Syria na Urusi.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman