1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani katika mazungumzo tete ya Syria

12 Aprili 2017

Baada ya Marekani kuishambulia Syria,Urusi inaukosoa utawala wa Trump na kusema unachukua hatua za mabavu zilopitwa na wakati

https://p.dw.com/p/2b6yg
USA Russland Tillerson bei Lawrow
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Msimamo wa Marekani kuelekea mgogoro huo wa Syria bado haujaeleweka nchini Urusi amenukuliwa akisema naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov ambaye pia amesema nchi yake hailewi mwelekeo wa kimabavu uliopitwa na wakati unaochukuliwa na Marekani.Kauli hiyo imechapishwa dakika chache tu kabla ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson ambaye ni mwakilishi wa ngazi ya juu kabisa katika utawala wa Donald Trump kuitembelea Urusi na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Urusi.

Wanadiplomasia hao wa Marekani na Urusi wameanza mazungumzo yao huku pande hizo mbili zikiwa katika hali ya wasiwasi mkubwa kati yao kutokana na suala la utawala wa Syria kulaumiwa kuhusika na mashambulio ya kutumia silaha za sumu na upande wa pili hatua iliyochukuliwa na Marekani kujibu mashambulio hayo kwa kufyetua makombora ya kasi nchini Syria.Serikali ya rais Trump imeishutumu Urusi Jana kwa kujaribu kuikingia kifua serikali ya Syria dhidi ya kulaumiwa kutokana na mashambulio hayo ya silaha za sumu yaliyosababisha maafa makubwa Syria.

Urusi kwa upande wake inaamini na kumtetea rais Assad ikisema  hakuna ushahidi unaoonesha kwamba ni vikosi vya Assad vilivyotumia gesi ya sumu kuua raia wasiokuwa na hatia nchini Syria na badala yake imezielekeza lawama hizo kwa makundi ya waasi. Kufuatia msimamo huo unaotafautiana kati ya Marekani na Urusi wasiwasi umeyagubika mazungumzo ya leo mjini Moscow ambayo naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabov amesema yatajikita zaidi katika kulijadili suala la kuwepo eneo la kuzuia urukaji wa ndege nchini Syria  pamoja na Korea Kaskazini na vile vile Ukraine.

Syrien Mutmaßlich Chlorin-Gas in Idlib eingesetzt
Picha: picture-alliance/dpa/M. Jalal/Syria Civil Defense Idlib

Wakati huohuo huko Syria kwenyewe mpango wa kuwahamisha wasyria walioko katika maeneo mbali mbali ya nchi yaliyozingirwa umeanza kwa kufanyika ubadilishanaji wa wafungwa.Hakim Baghdad mwanachama wa kamati ya msaada kwa ajili ya vijiji viwili  vilivyozingirwa na waasi kaskazinimagharibi mwa Syria amesema shughulia ya kuachiliwa wafungwa ilifanyika usiku ikisimamiwa na shirika la hilali nyekundu la Syria ingawa shirika hilo halijatowa taarifa yoyote hadi sasa.

Shirika la habari la linalosimamiwa na jeshi limesema waasi wamewaachia huru wanwake wanane watoto wanne na kuzitoa maiti za watu tisa.Kwa upande mwingine wanamgambo wanaoegemea serikali wamewaachia huru wapiganaji 19 na kutoa maiti moja.Mpango huo ni sehemu ya maridhiano ya kuhamishwa wakaazi  10,000 wa maeneo mawili yanayoshikiliwa na wapinzani karibu na mji wa Damascus na  vijiji viwili kaskazini mwa Syria,mpango ambao wakosoaji wanasema unazidisha idadi ya watu wanaolazimishwa kuyahama mkaazi yao.

Mwandishi:Mwasimba Saumu

Mhariri Josephat Charo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW