Urusi na Belarus zajiandaa kwa luteka kubwa ya kijeshi
29 Januari 2022Hayo ni kulingana na wizara ya ulinzi ya Urusi kupitia taarifa iliyotolewa leo siku ya Jumamosi.
Mfumo wa kujikinga na makombora ya masafa mafupi wa Pantisir-S tayari umewasili nchini Belarus kujiunga na ndege za kivita chapa Su-35 amabzo tayari zilikwishapelekwa nchini humo.
Wizara hiyo imesema pia mfumo wa ulinzi dhidi ya mashambulizi ya anga wa S-400 pia uko njiani kupelekwa nchini Belarus.
Mipango ya serikali mjini Moscow na Minsk ya kufanya luteka kubwa ya kijeshi nchini Belarus mnamo Februari 10 hadi 20 imezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa mataifa ya magharibi.
Mzozo unaondelea sasa kuhusu Ukraine ndiyo umechochea wasiwasi huo ikitiliwa maanan sehemu ya majaribio ya medani za kivita yaliyopangwa yatafanyika kusini mwa Belarus karibu na mpaka wa Ukraine.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imeelezea wasiwasi wake kwamba Moscow inaweza kupeleka wanajeshinwake nchini Belarus kwa kisingizio cha kufanya mazoezi ya kijeshi lakini mwishoye ikawatumia kuivamia Ukraine kutokea upande huo. Moscow imekanusha madai hayo.
Rais Joe Biden asema Marekani inapanga kupeleka wanajeshi zaidi Ulaya
Hayo yanajiri wakari rais Joe Biden amesema Marekani inapanga kutuma wanajeshi zaidi huko mashariki mwa Ulaya, wakati nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami NATO wakijaribu kuimarisha uwepo wao kama sehemu ya mkwamo wake na Urusi.
Biden alitoa kauli hiyo siku ya Ijumaa akisema kwamba atapeleka wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo katika siku za karibuni, akiongeza kuwa idadi yao haitakuwa kubwa.
Siku ya Jumatatu Biden aliamuru wanajeshi 8,500 kuwa katika hali ya utayari ili waweze kusambazwa endapo watahitajika.
Alisisitiza kwamba hatua hiyo ni ya tahadhari katika kushughulikia kero za wanachama wa NATO wa Ulaya Mashariki.
Hata hivyo Marekani haitopeleka wanajeshi wake ndani ya Ukraine yenyewe. Kwa kawaida Marekani ina maelfu ya wanajeshi wake barani Ulaya ikiwemo askari elfu 35,000 nchini Ujerumani.