Urusi, mataifa ya Magharibi uso kwa uso Baraza la Usalama
25 Aprili 2023Akiongoza kikao kilichokusudiwa kuwa mdahalo juu ya nafasi ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa katika ulimwengu wa sasa uliogawanyika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Segrei Lavrov, aliyatuhumu waziwazi mataifa ya Magharibi kwa kuitenga nchi yake na kusaka njia za kuidhibiti China.
Makhsusi kabisa, Lavrov aliilaumu Marekani kwa kutanguliza mbele maslahi yake pekee kwenye eneo la Bahari ya China Kusini na pia Muungano wa Kijeshi wa NATO kwa kupanga kuihujumu Urusi.
Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Urusi alionya kwamba nchi yake haitaruhusu tena kuchezewa maslahi yake kwa kutumia mataifa jirani na kuapa kwamba wataendelea na operesheni ya kijeshi dhidi ya Ukraine hadi malengo ya Moscow yatimie.
Soma zaidi: Guterres amependekeza njia ya kusafirisha nafaka ya Ukraine
"Urusi imeweka wazi malengo inayoyataka katika operesheni yake maalum ya kijeshi: kufekya vitisho kwa usalama wetu vilivyopandikizwa na NATO kwenye mipaka yetu kwa miaka kadhaa sasa; kuwalinda watu walionyimwa haki zilizotangazwa kwa matamko ya kimataifa, kuwalinda dhidi ya kitisho cha kuangamizwa na kufukuzwa kwenye ardhi ya wazee wao ambacho kimewekwa wazi na utawala wa Kyiv. Tumesema kwa nini na nani tunapigana naye." Alisema Lavrov.
Guterres aja juu
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliyekuwa amekaa kando tu ya Lavrov, alimwambia waziwazi mwakilishi huyo wa ngazi za juu wa Urusi, kwamba kwa kuivamia Ukraine, Moscow imeifanya dunia ikabiliwe na mzozo usio kifani, ambapo sasa mfumo wa mashirikiano ya kimataifa upo hatarini kuliko muda wowote tangu kuundwa Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema hivi sasa uhasama baina ya mataifa makubwa ni wa hali ya juu na akaonya juu ya uwezekano wa vita kutokana uvamizi ambao haukubaliki na ni kinyume cha mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Soma zaidi: Mawaziri wa Ulinzi wa Urusi, Iran, Uturuki na Syria wakutana Moscow
"Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, unaovunja Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, unasababisha mateso na fadhaa kwa nchi hiyo na watu wake. Na unaongeza mzigo kwenye uchumi wa dunia uliokwishaparaganyika kwa janga la UVIKO-19." Alisema Guterres.
Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yalitowa tamko lao muda mchache kabla ya kuanza kikao hicho cha Baraza la Usalama jijii New York, ambapo Mkuu wa Ujumbe wa Umoja huo, Olof Skoog, alisema lazima jumuiya ya kimataifa ichukuwe hatua madhubuti kuhakikisha "waliohusika na uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinaadamu nchini Ukraine wanawajibishwa."
Vyanzo: Reuters, AP