1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kutoa msaada zaidi wa kijeshi nchini Burkina Faso

5 Juni 2024

Urusi itatuma vifaa zaidi vya kijeshi na wakufunzi nchini Burkina Faso kuisaidia nchi hiyo kuimarisha uwezo wake wa ulinzi na mapambano dhidi ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/4gflM
Mali Unruhen Soldaten
Operesheni Barkhane iliyofanywa katika ukanda wa Sahel ikijumiisha eneo la mataifa ya Mauritania, Mali, Burkina Faso,Picha: Sebastien Rieussec/Hans Lucas/IMAGO

Haya yametangazwa leo na vyombo vya habari vya Urusi vilivyomnukuu waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Sergei Lavrov. Shirika la habari la TASS, limemnukuu Lavrov akiwa ziarani nchini Burkina Faso akisema kwamba tangu mawasiliano ya kwanza kati ya nchi hizo mbili baada ya Rais Ibrahim Traoré kuingia madarakani, wamekuwa wakishirikiana kwa karibu sana katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa kijeshi. Katika mkutano na waandishi habari mjini Ouagadougou, Lavrov ameongeza kusema hana shaka kwamba masalia ya ugaidi yaliyopo nchini Burkina Faso yataangamizwa. Lavrov amefanya ziara kadhaa barani Afrika tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine huku Urusi inayokabiliwa na vikwazo vya Magharibi, ikitafuta washirika wapya wa kibiashara na inajaribu kuhamasisha nchi zinazoendelea kukubaliana na mtazamo wa kuwa na ulimwengu wenye mfumo tafauti usiotawaliwa tena na Marekani na wakoloni wa zamani, Ulaya.