Urusi kupunguza operesheni za kijeshi karibu na Kyiv
29 Machi 2022Naibu Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Alexander Fomin amesema hatua hiyo ina lengo la kuongeza hali ya kuaminiana wakati wapatanishi wakikutana ana kwa ana, baada ya duru kadhaa za mazungumzo kushindwa kuzaa matunda yoyote. Ingawa hata hivyo vikosi vya Urusi katika siku za hivi karibuni vinaelezwa kukwama katika jitihada zake za kusonga mbele katika uwanja wa vita.
Mazungumzo ya Urusi yameibua matumani yaliofifia kwamba huenda kukapigwa hatua katika kuelekea kumaliza kampeni ya umwagaji damu katika ardhi ya Ukraine. Naibu Waziri Fomin amesema serikali ya Moscow kimsingi imeamua kupunguza shughuli za kijeshi kuelekea miji ya Kyiv na Chernihiv kwa lengo la kuongeza hali ya kuaminiana na kuweka mazingira ya mazungumzo zaidi baina ya Urusi na Ukraine.
Ishara ya kuondoka kwa majeshi ya Urusi katika miji ya Kyiv na Chernihiv
Jeshi la Ukraine limeonesha kubaini kuondoka kwa majeshi hayo katika maeneo ya karibu na Kyiv na Chernihiv, Ingawa wizara ya Ulinzi ya Marekani, imesema imeshindwa kuhakiki taarifa hiyo.
Mshauri wa rais wa Ukraine alisema mkutano huo wa leo huko Istanbul ulilenga katika kufanikishwa usitishwaji wa mapigano na dhamana ya kiusalama kwa Ukraine masuala ambayo kwa wakati wote yamekuwa kitovu cha mazungumzo yasiyofanikiwa ya kipindi kilichopita. Mevlut Cavusoglu ni waziri wa mambo ya nje wa Uturuki."Katika mkutano huu uliofanyika leo, tumeshuhudia hatua fulani zimepigwa. Awali mlizisikia kauli za wajumbe. Makubaliano na maelewano yamefikiwa katika baadhi ya masuala. Hatua za maana zaidi zimefikiwa leo tangu kuanza kwa majadiliano. Yale masuala magumu yatapelekwa katika ngazi za juu."
Akizungumza pia muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano huo kiongozi wa Ujumbe wa Urusi katika mazungumzo hayo, Vladimir Medinsky aliwaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo ya safari hii yamekuwa yenye tija. Na kuongeza kuwa taifa lake lipo tayari kuchukua hatua za kijeshi na kisiasa kupunguza mzozo huo.
Urusi haiwezi kupinga Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya
Kuhusu mapendekezo ya Ukraine, Medinsky amesema yatafanyiwa tathmini katika siku chache zijazo, kuwasilishwa kwa rais na watayajibu kwa kadri itakavyopaswa. Lakini moja ya hayo ni lile la Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya ambalo Urusi haiwezi kulipinga. Serikali ya Urusi imeaonesha ishara ya kutaka kuendelea kwa mazungumzo hayo.
Kabla ya duru hii ya mazungumzo ya sasa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy alisema taifa lake lipo tayari kutangaza kutoegemea upande wowote, kama inavyoshinikizwa na Urusi, na ipo tayari kuafikiana kuhusu eneo ya taifa hilo linalozozaniwa la upande wa mashariki la Donbas, kauli ambayo inaweza kutoa msukumo wa mazungumzo ya upatanishi kwa pande hizo hasimu
Vyanzo: DPA/RTR/AP.