Urusi: Kupelekwa makombora ya kisasa Ukraine ni tishio
18 Oktoba 2023Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, Putin amesema Marekani ilikuwa imefanya kosa kwa kuruhusu kuhusishwa kwa undani katika mzozo wa Ukraine na hivyo kurefusha mateso chini humo. Akizungumzia mfumo huo wa kijeshi wa Marekani, Putin amesema ni hatari na inaongezea tishio la ziada. Putin pia amesema kuwa watatibua mashambulizi hayo.
Ukraine yathibitisha kutumia makobora ya Marekani
Hapo jana Jumanne (18.10.2023) Ukraine ilithibitisha kwamba imefanikiwa kutumia makombora yalioletwa nchini humo na Marekani dhidi ya ngome za Urusi.
Leo Jumatano, waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu, amesema nchi hiyo imeanza kuimarisha usalama wa mpaka wake wa Magharibi kwa matarajio ya ndege za kivita aina ya F-16 zilizotengenezwa Marekani zitakazopelekwa Ukraine mwakani. Haya yameripotiwa na shirika la Habari la serikali ya Urusi RIA.
Mashambulizi ya Urusi yasababisha vifo vya watu watano
Katika hatua nyingine, mashambulizi ya Urusi ya usiku wa kuamkia leo na leo Jumatano (18.10.2023) yamesababisha vifo vya watu watano na kuharibiwa kwa gridi ya umeme katika mji wa Kaskazini Mashariki wa Kharkiv.
Haya ni kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine. Maafisa hao wamesema kuwa raia wawili waliuawa katika mashambulizi hayo ya asubuhi dhidi ya majengo ya makazi katika mji wa Kusini Mashariki wa Zaporizhzhia na mwanamke wa umri wa miaka 31 akauawa katika shambulizi dhidi ya Kijiji cha Obukhivka katika eneo la Kati la Dnipropetrovsk.
Soma pia:Raia wawili wauawa katika shambulizi la Urusi mjini Avdiivka nchini uKraine
Katika ujumbe kupitia mtandao wa Telegram, gavana wa eneo la Kherson Oleksandr Prokudin amesema mwanamke na mwanamume mmoja pia waliuawa katika shambulizi la usiku kucha katika eneo la Kusini la Kherson. Maafisa katika eneo la Kharkiv, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, wamesema gridi ya umeme ya eneo hilo iliharibiwa katika shambulio la Urusi na kukatika kwa umeme kunatarajiwa.
Zelensky asema vitisho vya Urusi lazima vishindwe
Katika ujumbe kupitia mtandao wa telegram, rais wa Ukraine Volodymr Zelensky amesema taifa hilo aliloliita ovu linaendelea kutumia vitisho na kushambulia raia. Zelensky ameongeza kuwa vitisho vya Urusi lazima vishindwe. Rais huyo pia alichapisha picha ya jengo la ghorofa tano mjini Zaporizhzhia likiwa na shimo la katikatika , lango lake kuharibiwa, madirisha kuvunjika na likiwa limezungukwa na uchafu.