Urusi: Marekani yachochea uvunjaji sheria kuhusu maandamano
24 Januari 2021Dmitry Peskov amesema hayo Jumapili, siku moja tu baada ya maandamano kufanyika katika miji mbalimbali nchini Urusi kushinikiza kiongozi wa upinzani ambaye pia ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Urusi, Alexei Navalny ambaye kuachiliwa huru.
Wakati wa maandamano, msemaji wa ubalozi wa Marekani Rebecca Ross alisema kupitia ukurasa wa Twitter kwamba Marekani inaunga mkono haki ya watu wote kushiriki maandamano ya amani na haki ya kila mtu kujieleza.
Soma pia: Polisi Urusi yawakamata zaidi ya wafuasi 3,400 wa Navalny
Ross aliongeza kwamba hatua zinazochukuliwa na maafisa wa Urusi zinakandamiza haki hizo. Ubalozi huo pia uliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya kutaka Navalny aachiliwe huru.
Peskov amesema kauli hizo zinaingilia kati masuala ya ndani ya Urusi na kwa namna fulani zinachochea ukiukwaji wa sheria ya shirikisho la Urusi na zinaunga mkono matendo ambayo hayajaruhusiwa.
Wito watolewa Umoja wa Ulaya kumwekea Putin vikwazo vya kifedha
Wakati hayo yakijiri, afisa mmoja mkuu wa Umoja wa Ulaya ametaka umoja huo kumuadhibu rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kumuwekea vikwazo vya kifedha kufuatia hatua ya maafisa wake wa polisi kuwakamata maelfu ya wafuasi wa Navalny.
Manfred Weber ambaye ni mwanasiasa wa Ujerumani anayeongoza kundi la wabunge wanaoegemea siasa za mrengo wa kati kulia katika bungee la Umoja wa Ulaya (EPP) ameliambia gazeti la Ujerumani RND kwamba hatua ya Urusi kuwakamata waandamanaji haikubaliki.
Weber amesema mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya hawapaswi kukwepa kulijadili suala hilo kwa mara nyingine.
EU yataka mradi wa bomba la gesi Nord Stream 2 usitishwe
Mnamo Alhamisi, wabunge wa Umoja wa Ulaya walipitisha azimio la kutaka kusitisha mradi wa bomba la gesi Nord Stream 2 kati ya Urusi na Ujerumani kama jibu kufuatia kukamatwa kwa Navalny.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye ameendelea kuunga mkono mradi huo licha ya ukosoaji ndani ya Umoja wa Ulaya, alisema mtizamo wake haujabadilika licha ya kesi ya Navalny.
MArekani, Umoja wa Ulaya na Uingereza zimeshutumu vikosi vya usalama vya Urusi kwa namna ambnavyo vilishughulikia maandamano ya Jumamosi.
(APE, RTRE)