1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi imejiondoa katika mkataba wa nafaka

18 Julai 2023

Urusi imeshambulia bandari ya Ukraine ya Odesa kwa makombora na ndege zisizokuwa na rubani siku moja baada ya kujiondoa katika mpango unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wa kuruhusu Kyiv kuuza nje nafaka.

https://p.dw.com/p/4U3jB
Ukraine meldet neue russische Drohnenangriffe
Picha: UKRAINIAN ARMED FORCES/REUTERS

Mashambulizi ya Urusi kwenye bandari za Ukraine yanajiri baada ya Moscow kuahidi kulipiza kisasi mashambulizi ya barabara ya daraja linaloiunganisha Urusi na rasi ya Crimea.

Soma pia: Mkataba wa nafaka wafikia kikomo baada ya kujiondoa kwa Urusi

Muda mfupi baada ya daraja hilo kushambuliwa jana Jumatatu, Moscow ilijiondoa katika mkataba wa mwaka mmoja wa Umoja wa Mataifa wa mauzo ya nafaka, hatua ambayo Umoja wa Mataifa umeitaja kama hatari ya itakayayosababisha njaa duniani kote.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine, Andriy Yermak amesema mashambulizi ya Urusi kwenye bandari za Ukraine yalikuwa kile alichokitaja kuwa "ushahidi kwamba nchi gaidi"  inataka kuhatarisha maisha ya watu milioni 400 katika nchi mbalimbali ambazo hutegemea Ukraine kwa mauzo ya chakula.

Soma pia: Urusi yakataa kurefusha mkataba wa nafaka, dunia yalalamika

Jeshi la anga la Ukraine limesema wamedungua makombora sita aina ya Kalibr na ndege zisizokuwa na rubani 31 kati ya 36, zilizoelekezwa kwenye pwani ya Odesa na mikoa ya kusini ya Mykolaiv.

Ujerumani ina jukumu katika kusitisha vita

Nigeria | Rückgabe der Benin-Bronzen in Abuja
Annalena BaerbockPicha: Annette Riedl/dpa/picture alliance

Akizungumza na DW ya kando ya sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu kuundwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC),Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbockalisisitiza umuhimu wa kumshinikiza Putin kutengua uamuzi huo, akisema njia bora zaidi ni kwa nchi waagizaji za Afrika,Amerika Kusini, Asia, kuzungumza na Putin moja kwa moja.

Baerbock ameongeza kusema kwamba Ujerumani ina awajibu wa kuzuia vita kwa sababu ilihusika na uhalifu mkubwa zaidi duniani katika siku za nyuma.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, amekosoa hatua ya Urusi kusitisha mkataba huo kwa kusema:

"Urusi inayaweka mataifa mengi barani Asia na Afrika katika hatari ya kukabiliwa na ongezeko la bei ya chakula na njaa. Hii lazima ikome. Na sasa, unajua, sisi sote tunatatizika; tunapaswa kutatua tatizo lingine lililoundwa na Urusi. Na nilisisitiza kwa Katibu Mkuu, na ninasisitiza pia katika mazungumzo yote, kwamba 'tukiwa na utashi wa kisiasa, tutatafuta njia.' kwa mashauriano ya kina katika ngazi zote ili kupata suluhu la tatizo hili kubwa ambalo Urusi imetengeneza kwa dunia.”

Mkataba huu mauzo ya nafaka wa Bahari Nyeusi uliandaliwa mwaka mmoja uliopita na Uturuki na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo Urusi imesema makubaliano hayo yalikuwa hayazinufaishi nchi maskini hasa za bara la Afrika.