Upinzani wapendekeza serikali ya muungano Burundi
23 Julai 2015Wito huo umetolewa na Agathon Rwasa ambaye amemtaka Rais Nkurunziza kuitisha mazungumzo na wapinzani na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kufuatia uchaguzi wenye utata. Rwasa amesema pendekezo lake hilo linaweza kusaidia kurejesha amani nchini humo.
Rwasa, ambaye kama Rais Nkurunziza aliwahi kuwa muasi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kuna ulazima wa hatua za haraka kuchukuliwa hivi sasa ili kuwazuwia majenerali waliopanga jaribio la mapinduzi la Mei kuzusha tena vurugu wakati ambapo tayari nchi hiyo imo katika mzozo wa kisiasa uliosababishwa na uamuzi wa Rais Nkurunziza kugombea muhula wa tatu madarakani.
Upinzani unamlaumu rais huyo kukiuka katiba kwa kugombea muhula wa tatu na hivyo ulisusia uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne (21 Julai) jambo ambalo linampa nafasi kubwa Nkurunziza kuibuka na ushindi. Kwa upande wake, Nkurunziza amekanusha kuvunja sheria yoyote, akisema uamuzi wa mahakama unamruhuusu kugombea tena urais kwa mara ya tatu. Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa wiki hii.
Nkurunziza akubali pendekezo
Mshauri wa Rais Nkurunziza, Willy Nyamitwe, amesema kiongozi huyo hatapinga pendekezo la serikali ya umoja wa kitaifa na kuongeza kuwa serikali iko tayari kwa hilo lakini haitokubali kufanya hivyo kwa masharti yoyote.
Rwasa, kiongozi wa umoja wa upinzani wa Amizero y'Abarundi, aliiambia Reuters kwamba kuna baadhi ya wapinzani ambao tayari wameshatishia mapigano ya kutumia silaha. Rwasa amesisitiza kuwa kwa masilahi ya Warundi, serikali ya muungano wa kitaifa ni suluhisho litakaloweza kukubalika.
Halikadhalika, mmoja wa majenerali waliohusika na jaribio la mapinduzi ya Me, ameiambia Reuters kuwa matumizi ya nguvu ndio njia pekee iliyosalia ya kumuondoa Nkurunziza, baada ya njia za mazungumzo na shinikizo la kimataifa kushindwa kumzuia kugombea muhula wa tatu madarakani.
Mgogoro huu wa sasa, ambao ni mbaya zaidi tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2005, umeleta mvutano mkubwa nchini Burundi ambayo iko katika eneo lenye historia ya vita vya kikabila.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba