Upinzani Tanzania watoa wito wa maridhiano kisiasa Tanzania
9 Desemba 2019Viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania wametoa rai ya kufunguliwa kwa ukurasa mpya wa siasa za maridhiano nchini humo. Matamshi hayo wameyatoa leo mbele ya Rais wa Tanzania, John Magufulu wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika.
Wakati maelfu ya Watanzania wakikusanyika katika uwanja wa CCM KIRUMBA, mjini Mwanza kusherehekea miaka 58 ya Uhuru wa Tangayika, viongozi wa vyama vya siasa wameitumia siku hii mbele ya Rais Magufuli na maelfu ya Watanzania kuomba maridhiano ya kisiasa, kulindwa kwa demokrasia na uhuru wa kujieleza. Wito huo umetolewa na Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema.
Wakati Mbowe akiitumia nafasi hiyo kusisitiza haja ya kuwepo kwa mazungumzo yanayolenga kufungua ukurasa mpya wa siasa nchini Tanzania, mwenyekiti wa chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ametaka uwanja wa siasa na maendeleo nchini Tanzania kuwa sawa kwa pande zote husika.
Kwa upande wake Rais John Magufuli mbali na kuelezea mafanikio ya nchi tangu mwaka 1961, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuhakikisha inalinda tunu za Uhuru wa Tanganyika huku akiwataka Watanzania kuwa wamoja.
Mbali na kuwahakikishia Watanzania kuzilinda tunu za taifa, Rais Magufuli ametumia nafasi hii kutoa msamaha kwa wafungwa 5,532, mahabusu 345 na wale waliokwa wakituhumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi 256. Sherehe za uhuru za mwaka huu zimehudhuriwa na viongozi wote wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na viongozi wa kimila.