Upinzani Tanzania watoa maoni kuhusu uchaguzi wa Kenya
11 Agosti 2022Vyama hivyo vimekaribisha hatua inayochukuliwa na Tume Huru na Mipaka ya Kenya jinsi inavyowasilisha matokeo ya uchaguzi mkuu huku vikionekana kukosoa mifumo iliyoko nchini Tanzania vikisema kwa kiasi kikubwa mifumo hiyo inatoa upendeleo kwa chama kilichoko madarakani kuendelea kuongoza dola.
Baadhi ya vyama hivyo vinasema, mazingira ya upigaji kura, uhesabuji wa matokeo hadi hatua ya mwisho ya ujumulishaji wake ni maeneo yanayokosa uwazi kwa chaguzi nyingi za Tanzania hali ikiwa tofauti wa taifa hilo jirani la Kenya ambalo uchaguzi wake unafuatiliwa kwa kiwango kikubwa nchini.
Mmoja wa viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini, John Mrema ambaye ni mkurugenzi wa itifaki na mawasiliano wa CHADEMA amesema, Tume ya taifa ya uchaguzi ya Tanzania inapaswa kuweka wazi sikio lake kujua kile kinachoendelea kushuhudiwa nchini Kenya.
Uchaguzi wa Kenya wachagiza mjadala wa Tume huru na Katiba nchini Tanzania
Katika wakati huu kukiwa na mjadala mkubwa wa kitaifa kuhusu kipi kianze kati ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, chama cha ACT-Wazalendo kinasema wimbo wake wa kutaka mchakato wa katiba mpya utanguliwe kwanza na tume huru ya uchaguzi, unadhirika kupitia kile kinachofanywa na tume ya Kenya.
Naibu Katibu mwenezi ACT Wazalendo Taifa, Janeth Rithe analimulika jambo hilo akisema tume huru ya uchaguzi ndiyo mwarobaini utakaosaidia kuleta hisia za uwazi wakati wa uchaguzi.
Vyama vya upinzani mara zote vimekuwa vikikosoa kuhusu kukosekana kwa uwazi wakati wa uchaguzi mkuu na vingi vyao vinatolea mfano uchaguzi uliopita wa mwaka 2020 wanaodai ulichakachuliwa.
Mbali ya uchaguzi huu, vyama hivyo pia vinaukosoa uchaguzi wa mwaka mmoja nyuma yaani ule wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2019 ambao ulisusiwa na baadhi ya wagombea wa upinzani.