Upinzani Tanzania wataka majibu kuhusu ziliko trilioni 1.5
19 Aprili 2018Chama cha ACT wazalendo nchini Tanzania kimesema licha ya majibu dhaifu ya chama cha mapinduzi CCM kuhusu ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG, pia wana nia ya kuhamisha mjadala walioutaja kuwa ni wa kitaifa, wa upotevu wa shilingi trillion 1.5. Hayo ni kwa mujibu wa katibu wa itikadi na uwenezi wa chama hicho Ado Shaibu alipozungumza na waandishi wa habari mapema leo na kuongeza kuwa chama tawala CCM kimetengeneza takwimu ambazo hazipo kwenye ripiti ya CAG, kwa lengo la kuwadanganya wananchi.
Mjadala kuhusu ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG umeendelea kushika hatamu miongoni mwa wananchi wa kawaida, wasomi,na wachumi huku wanasiasa hasa kutoka vyama vya upinzani wakiwa bado wanataka majibu thabiti juu ya kiasi cha shilingi trillion moja na bilioni mia tano huku mawaziri wakitumia nguvu nyingi kuikosoa ripoti hiyo, huku chama tawala CCM kikisema kuwa ACT kinafanya upotoshaji kwa wananchi.
Hata hivyo chama hicho kimesema kuwa, ukaguzi wa CAG ulihusu fedha zilizokusanywa si mapato ghafi wala fedha tarahiwa na hakuna fedha za serikali ya zanzibar kutokana na kutokuwepo kwa nyaraka yoyote inayoonesha makusanyo ya fedha za zanzibar.
Ado Shaibu ambae ni katibu wa itikadi na uwenezi wa chama cha ACT wazalendo amewaambia waandishi wa habari kuwa, CAG ameonesha mapungufu Makubwa ya serikali kiasi cha serikali kupika takwimu ili ipate sifa kuwa inafanya vizuri.
Kwa mujibu wa ukokotoaji wa ACT wazalendo kiasi cha shilingi trillion moja na bilioni mia tano zingeweza kukopesha shilingi milioni 100 kwa vijiji 15000 kwa nchi nzima, kutatua tatizo la mitaji kwa vijana na wanawake na hata zingeweza kujenga hospitali 10 zenye hadhi ya Mloganzila na kusomesha bure vijana wa chuo kikuu wanaoomba mikopo kwa muda wa miaka minne mfululizo
Hata hivyo Ado amesema kuwa ikiwa hii ndio ripoti ya kwanza ya CAG kwa serikali ya awamu ya tano na imeonesha madhaifu makubwa ni wazi wananchi wategemee hasara zaidi endapo hawataendelea kuhoji juu ya trillion moja na bilioni mia tano zilipo.
Kadhalika ameongeza kuwa nguvu inayotumiwa na CCM kuhamisha mjadala alioutaja wa kitaifa na kuuweka katika sura ya kisiasa ni mbinu dhaifu na haina mashiko dhidi ya nguvu ya umma.
Kwa kutanua mjadala chama hicho kimekwenda mbali zaidi na kumuandikia spika wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania barua kuomba uchunguzi maalum na huru kufannywa na ACG kuchunguza upotevu wa fedha hizo.
Mwandishi: Hawa Bihoga
Mhariri:Josephat Charo