Upinzani Tanzania wakosoa utaratibu wa kujiuzulu kwa Ndugai
7 Januari 2022Wakiwa katika mikutano na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama vya upinzani wanasema kitendo cha Job Ndugai kuachia ngazi kwenye nafasi yake kinadhihirisha namna mhimili wa Bunge ulivyokuwa dhaifu na kushindwa kusimama katika nafasi yake.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia amesema kimsingi Ndugai amekwenda kinyume na matakwa ya Katiba inayosema iwapo spika atataka kujiuzulu basi atafanya hivyo mbele ya wabunge na siyo kama alivyofanya kwa kumwandikia barua katibu mkuu wa chama tawala CCM.
Mwenyekiti huyo ambaye anasema ana uzoefu wa kuwa bungeni kwa zaidi ya miaka 15, analaumu namna mhimili wa serikali kuu kuingilia utendaji wa mihili mingine akitolea mfano hatua ya Ndugai kukoselewa na kushinikizwa ajiuzulu kwa vile tu alijitokeza hadharani kuzungumzia deni la taifa.
Soma pia:Spika wa Bunge la Tanzania amejiuzulu
CHADEMA yalaani uingiliaji kati wa serikali
Akiwa ughaibuni anakoishi kwa sasa, makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anasema ingawa hakufurahishwa na utendaji wa Ndugai kama spika, lakini hii haimainishi kwamba njia ya kujiuzulu kwake isikosolewe.
Anaona kwamba mhimili huo wa bunge umekuwa ukiingiliwa mara kwa mara na mara zote unatumika kama mhuri wa kupitisha ajenda za serikali kuu. Anasisitiza kuwa, haya yanayojitokeza sasa yanapaswa kuwa kama funzo kukoleza mjadala wa kupatikana kwa katiba mpya.
Hatua ya Ndugai ambaye sasa anasalia kuwa mbunge wa kawaida wa Kongwa, kuachia nafasi yake imetokea baada ya kupingwa vikali na Rais Samia Suluhu Hassan aliyeonyesha kutoridhishwa kwake na namna kiongozi huyo alivyozusha mjadala kuhusiana na serikali kuendelea kukopa.
Ama taarifa ya katibu wa bunge iliyotolewa leo mchana imeahirisha vikao vya kamati za bunge vilivyotarajiwa kuanza Jumatatu ijayo, na badala yake taarifa hiyo imewataka wabunge wote kuwasili bungeni Januari 31 kujiandaa na vikao vya kawaida vya bunge.