Upinzani Syria wakubali kuhudhuria mkutano wa Geneva II
19 Januari 2014Muungano wa kitaifa ambao umegawika kwa kiasi kikubwa umekuwa katika mbinyo mkali wa kimataifa kuhudhuria mkutano huo , ambao una lengo la kutafuta njia ya kutoka katika mzozo wa kinyama ambao umesababisha kiasi ya watu 130,000 kuuwawa na kusababisha mamilioni ya watu kubaki bila makaazi tangu Machi 2011.
Serikali ya Syria tayari imesema kuwa itahudhuria , licha ya kuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ameushutumu utawala huo kwa kufanya mbinu za kugawanya , akisema "hakuna mtu atakayedanganyika".
Muungano huo wa kitaifa ambao viongozi wake wanaishi uhamishoni limepiga kura 58 dhidi ya 14 pamoja na kura mbili ambazo hazikupigwa na moja imeharibika katika mkutano mjini istanbul kuunga mkono azimio la kuhudhuria kile kinachojulikana kama mazungumzo ya Geneva mbili, ambayo yanaanza rasmi siku ya jumatano.
Hii ina maana wajumbe 75 tu kati ya kiasi ya wajumbe 120 walishiriki katika upigaji huo wa kura, katika ishara kuwa bado kuna hali ya kutokubaliana. Kiongozi wa muungano huo Ahmad Jarba amesema kuwa kundi hilo linalounganisha makundi mbali mbali litahudhuria katika lengo moja la kumuondoa madarakani rais Assad. "Majadiliano ya Geneva mbili ni njia ya mwelekeo mmoja yenye lengo la kufanikisha madai yote ya mapinduzi, na muhimu zaidi likiwa la kumuondoa madarakani muuaji (Assad)," amesema.
Uamuzi wakaribishwa
Mataifa ya magharibi yameukaribisha uamuzi huo wa upande wa upinzani , ambao Kerry amesema "ni kwa ajili ya maslahi ya watu wa Syria ambao wametaabika kwa kiasi kikubwa chini ya utawala wa kinyama wa (Bashar al-Assad)". Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague ameusifu upinzani kwa kufikia kile alichokiita "uamuzi mgumu".
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema uamuzi huo unatoa "mwanga wa matumaini" kwa watu wa Syria na mwenzake wa Ufaransa Laurent Fabius ameuita uamuzi huo "chaguo la kijasiri".
Zaidi ya nchi 35 zitajumuika katika miji ya Uswisi ya Montreux na Geneva Jumatano wiki ijayo kwa ajili ya mazungumzo ya kuunda serikali ya mpito itakayoiongoza nchi hiyo, kama ilivyokubaliwa katika makubaliano ya mwaka 2012.
Muungano huo , ambao unajumuisha makundi mbali mbali, umekuwa ukihangaika kuweza kupata msimamo mmoja katika wakati wa vita vya nchi hiyo, ambapo ulitikiswa na mivutano ya ndani kuhusu uongozi na juhudi wa kuunda serikali iliyoko uhamishoni.
Wanachama wengi wa muungano huo wamekerwa na wazo la kukaa meza moja na wawakilishi wa utawala unaochukiwa ambao wamekuwa wakijaribu kuuondoa kutoka madarakani kwa zaidi ya miaka mitatu.
Pendekezo la maridhiano
Katika hatua ya kushangaza mjini Moscow siku ya Ijumaa, waziri wa mambo ya kigeni wa Syria Walid Muallem waliwasilisha kwa mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov mpango wa amani wenye lengo la kusitisha "hatua zote za kijeshi"katika mji wa kaskazini ulioharibiwa kwa vita wa Aleppo.
Muallem pia amesema utawala huo unaridhia kubadilishana wafungwa na waasi katika mabadilishano ya kwanza kama hayo tangu mzozo huo kuzuka, wakati Lavrov akisema Syria iko tayari kuchukua "hatua muhimu za kiutu" kuwezesha misaada kufika kwa walengwa.
Na jana Jumamosi (18.01.2014), chakula cha msaada kilifika katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina iliyozingirwa ya Yarmuk mjini Damascus, ambako dazeni kadha za watu wanaripotiwa kufariki kwa njaa na kukosa huduma ya madawa, kwa mara ya kwanza katika muda wa miezi minne.
Syria, amesema Muallem , itafanya "kila juhudi kuhakikisha kuwa mkutano wa Geneva mbili unafanikiwa na unatimiza matakwa ya watu wa Syria na maelekezo ya moja kwa moja ya rais Bashar al-Assad".
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Bruce Amani