Upigaji kura wamalizika kwa amani Zimbabwe
30 Julai 2018Miongoni mwa waliopiga kura zao ni mwenyewe Mugabe, ambaye hapo jana aliapa kamwe asingelikipigia chama chake cha ZANU-PF anachokishutumu kumuondosha madarakani kwa nguvu, huku mgombea wa upinzani, Nelson Chamisa, akisema kulikuwa na jitihada maalum za kuwahujumu wafuasi wake kutokana ucheleweshaji wa vifaa vya kupiga kura.
Rais huyo wa zamani alipiga kura yake kwenye kitongoji kimoja cha mji mkuu, Harare, ikiwa ni mara yake ya kwanza kupiga kura kwenye karatasi isiyokuwa na picha yake kama mgombea.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 94 na mmoja wa wakongwe wa siasa za Afrika, hakuzungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kwenye kituo cha kura, akisindikizwa na mkewe, Grace. Umma mkubwa ulikuwepo nje ya kituo hicho, wengine wakimshangiria na wengine wakimzomea.
Kauli yake ya jana iliyoashiria kwamba angelimpigia kura mgombea urais wa upinzani, Nelson Chamisa wa Vuguvugu la Demokrasia, MDC, iliwashangaza wengi, akiwemo Rais Emmerson Mnagangwa, ambaye haraka sana alimtuhumu Mugabe kwa kupanga mipango na Chamisa.
Usiku huo huo wa jana, vyombo vya habari viliripoti kuwa serikali imemuondolea ulinzi Mugabe kwenye jumba lake la kifakhari mjini Harare.
Chamisa alalamikia "hujuma za makusudi"
Mapema asubuhi, kiongozi wa upinzani, Chamisa, alipiga kura yake, huku akilalamikia kuwepo kwa njama za makusudi za kuwavunja moyo wafuasi wake, baada ya kuripotiwa matukio kadhaa ya ucheleweshaji vifaa vya kura vituoni.
Hata hivyo, aliita siku ya leo kuwa ni siku ya ushindi kwa Wazimbabwe.
"Watu wametoa kauli yao. Watu wana usemi wa juu na ni wazi kwamba kura hii ni kura kwa ajili ya ushindi, kwa ajili ya uhuru, demokrasia, Zimbabwe mpya, kura kwa ajili ya mwelekeo mpya. Sina wasiwasi kwamba hatimaye tutaweka bayana msisitizo wa sauti yetu kwa ajili ya mabadiliko, kwa ajili ya mwanzo mpya na kwa ajili ya vijana. Hiyo ndiyo sauti ninayoiwakilisha."
Hata hivyo, waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari walisema kwamba kwa ujumla upigaji kura ulikwenda kwa amani takribani nchi nzima. Misururu mirefu ilishuhudiwa kwenye vituo vingi mjini Harare, na tume ya uchaguzi ilisema kuwa wakati wa kufungwa vituo saa moja kamili magharibi, walioko kwenye mstari wangeliruhusiwa kupiga kura zao.
Baadhi ya waangalizi wa uchaguzi huo wameyasifia mazingira ya utulivu wakati wa kampeni na upigaji kura, lakini wameonesha wasiwasi wao kutokana na vyombo vya habari vya serikali kuelemea upande mmoja, ukosefu wa uwazi kwenye uchapishaji wa karatasi za kura na kuwepo kwa ripoti za vitisho kutoka kwa viongozi wa serikali ngazi za chini dhidi ya wafuasi wa upinzani.
Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe, ambayo ilikuwa ikishutumiwa kwenye chaguzi zilizopita kwa kuendesha wizi wa kura kumsaidia Mugabe, ilisema kuwa uchaguzi wa leo ulikuwa huru na wa haki. Watu milioni 5 na nusu walijiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa leo (Julai 30), huku wagombea urais wakipindukia 20, na vyama vya kisiasa takribani 130 vikishiriki.
Ikiwa hakuna mgombea wa urais atakayepata asilimia 50 ya kura, basi duru ya pili ya marudio itafanyika tarehe 8 Septemba.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf