1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNIFIL: Jeshi la Israel linaharibu mali zetu kwa makusudi

9 Novemba 2024

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon umelituhumu jeshi la Israel kuwa linafanya uharibifu wa kudhamiria wa mali na miundombinu yake.

https://p.dw.com/p/4moy5
UNIFIL Lebanon
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL.Picha: picture alliance/dpa

Ujumbe huo unaofahamika kwa kifupi kama UNIFIL, umesema matingatinga matatu yanayomilikiwa na jeshi la Israel yaliharibu sehemu ya uzio na ukuta wa kituo chake kimoja kwenye eneo la mpaka la Ras Naqoura siku ya Alhamisi.

Ujumbe huo umekitaja kisa hicho kiwa "ukiukaji usio mfano" wa sheria ya kimataifa. Kwenye taarifa yake kupitia mtandao wa kijamii wa X, UNIFIL imesema tukio hilo kama ilivyo kwa mengine 7 yanayafanana halikutokea kwa bahati mbaya na badala yake ni matendo ya wazi na ya makusudi yaliyofanywa na jeshi la Israel.

Kupitia tamko lake, UNIFIL imeikumbusha Israel kwamba inayo jukumu la kuhakikisha usalama kwa wafanyakazi na mali za Umoja wa Mataifa na mara zote kuheshimu maeneo yanayotumiwa na taasisi hiyo.